Rais wa Uganda Yoweri Museveni kwa mara nyingine amekosoa uondoaji wa ufadhili wa Benki ya Dunia, akisema kuwa shirika hilo linajidanganya ikiwa linadhani kwamba hatua hiyo itawatia hofu Waganda.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye akaunti yake ya X (zamani ya Twitter) siku ya Alhamisi, Bw Museveni aliitaja Benki ya Dunia kama “waigizaji wa kibeberu wasio na akili na wasiojua pa kuacha”.
Wiki iliyopita, Benki ya Dunia ilisitisha ufadhili kwa Uganda kwa sababu ya sheria tata ya kupinga ushoga iliyopitishwa mwezi Mei, ambayo ilikinzana na maadili ya Benki ya Dunia.
Sheria hiyo imeibua ukosoaji wa kimataifa kwa ukali wake, ikiwa ni pamoja na adhabu ya kifungo au kifo kwa watu wanaojihusisha na vitendo fulani vya jinsia moja.
Akijibu Benki ya Dunia wiki jana, Bw Museveni aliishutumu kwa kujaribu kuishinikiza Uganda kubadili sheria kwa kusitisha ufadhili, lakini akaongeza kuwa Uganda itaendelea kujiendeleza hata bila msaada wa Benki ya Dunia.
Mnamo Alhamisi, Bw Museveni alikariri kwamba ufadhili ulioondolewa hautazuia mabadiliko ya kiuchumi ya Uganda.
Aliongeza kuwa hatua kali ya Benki ya Dunia, kwa kweli, itasaidia jitihada za Uganda kupunguza deni la nje na kujitegemea zaidi.
Bw Museveni alisema Uganda bado ina washirika kadhaa wa Magharibi, lakini akasema wanatishwa na kuendelea kuiunga mkono Uganda.