Mvua ya upepo mkali yaezua nyumba 31 na kujeruhi watoto wawili nchini Tanzania

Mvua iliyo ambatana na upepo mkali imeharibu nyumba 31 katika kijiji cha Tukoma, Kata ya Itenka halmashauri ya Nsimbo mkoani Katavi hali iliyopelekea baadhi ya familia kulala nje huku nyingine zikikosa kabisa makazi.

Akitoa taarifa mbele ya kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Mpanda, Afisa mtendaji wa Kata ya Itenka Yegela Samike amesema mvua hiyo ilinyesha Novemba 9, 2022 majira ya saa 12:45 jioni.

Samike amesema pamoja na nyumba kuezuliwa na kubomoka, watoto wawili wa familia moja walijeruhiwa baada ya kudondokewa na matofali na hali zao zinaendelea vizuri.

Aidha amesema mifugo kama kuku na bata ambao idadi yake haijafahamika wamefunikwa na vifusi ikiwemo kuangukiwa na nyumba.

Kwa upande wao waathiriwa wa tukio hilo ambao wengi wao wamekosa makazi wameiomba serikali kuwasaidia kuezeka nyumba zao ili waweze kupata mahali pa kuishi.

Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Jamila Yusuph akiambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya hiyo ametoa pole kwa waathirika na kuahidi kuwa serikali inafanya tathmini za athari zilizosababishwa na tukio hilo ili kuona namna ya kusaidia.

Hata hivyo amewashauri kujenga nyumba bora ili kuepusha madhara ambayo yanaweza kuepukika sanjari na kupanda miti katika maeneo yao ili kuzikinga nyumba dhidi ya upepo mkali.

Tukio hili ni la kwanza kutokea tangu mvua  msimu wa kilimo 2022/2023  uzinduliwe  mkoani Katavi.