Wakili Boniface Mwabukusi amesema Serikali kusaini mikataba midogo mitatu na kampuni ya Dp World ya Dubai ni kuwalaghai wananchi kwa madai kuwa bado matatizo yako palepale katika mkataba mama wa IGA.
Mwabukusi amesema hayo jijini Mbeya ikiwa ni siku chache zimepita tangu Serikali isaini mkataba na DPW katika uendelezaji wa Bandari ya Dar es Salaam.
Mwabukusi ameeleza masikitiko yake kwa Serikali kusaini mkataba na DPW ya Dubai katika uendelezaji wa bandari ya Dar es Salaam akidai kuwa bado mapungufu hayajaondolewa na hata kipindi cha miaka 30 ya mkataba huo ni kirefu ikilinganishwa na raslimali inayoenda kuwekezwa.
“Kuna kitu kinaitwa IGA (Intergovernmental Agreement na kuna kitu kinaitwa HGA, tunaposema IGA ni ule mkataba mama ile Document yote inayotoa frame work au inayotoa mipaka, ukubwa na mawajibiko ya kila upande kwa ujumla wake kati ya Tanzania na Dubai. HGA ni mikataba mahususi kwa ajili ya matukio fulani hii inaitwa Host Government Agreement, kwahiyo mikataba hii ni mikatana inayozalishwa kulingana na Mkataba wa IGA. Kwa hiyo HGA ni kamkataba kadogo wa IGA”, Amesema wakili Mwabukusi na kuongeza.
“Sasa juzi (Oktoba 22, 2023) Serikali inasema imesikia maoni ya wananchi na kurekebisha mkataba (Mkataba wa bandari), Serikali imewadanganya wananchi kwa sababu moja IGA ndio iliyokuwa inalalamikiwa na tuligusa vipengele vyenye mapungufu ikiwemo uwezo wa Dubai, kukiuka sheria za ndani (Tanzania), ikiwemo kutwaa au kuweka mali chini ya mikono ya kigeni bila ukomo unaoeleweka. Sasa leo Serikali inazungumzia Host Government Agreement (HGA) halafu inawadanganya wa-Tanzania kana kwamba imerekebisha IGA hiyo si kweliIGA na HGA ni vitu viwili tofauti na HGA haiwezi kukiuka masharti ya IGA kwasababu IGA ndio mkataba mama, IGA ni Katiba na HGA ni kanuni sasa ukitwambia HGA ina miaka 30 je IGA ina miaka mingapi”, Ameeleza Wakili Mwabukusi.
Wakili Boniface Anyisile Mwabukusi amewataka wa-Tanzania kuungana kwenye masuala yanayohusu Taifa lao ikiwemo kufanya maandamano ya amani yatakayozinduliwa Novemba 09, 2023 mkoani Mbeya ili kufikisha ujumbe wao kwa Serikali kuwa hawakubaliani na mkataba wa Bandari.
“Kwahiyo kimsingi hakuna chochote kilichofanyika kwenye IGA, IGA haramu bado iko palepale walichofanya juzi ni ujanja na kucheza na maneno ya kuwachanganya wa-Tanzania wanaofikiri miaka 30 ni michache, utampaje mtu miaka 30…bado ni mingi katika uwekezaji tunaotaka utampaje asilimia 40 sisi asilimia 60 kwani sheria inasemaji, Sheria yetu (ya maliasili) inasema maliasili za asili zinakuwa mikononi mwa Umma kwahiyo kama unataka uwekezaji unaenda kwenye taasisi zinazoshikamana na Umma sio taasisi za kigeni na unazipa asilimia 40”, Amesema Wakili Mwabukusi.
Wakili huyo ameitaka Serikali kuweka wazi mkataba uliosainiwa ikiwa hauna shida yoyote huku akidai mapungufu bado yatakuwepo kwenye mkataba mama (IGA).
“Mimi nimewasikia (Serikali) na ninaweka tahadhari kwahiyo usiniulize nazungumzia wapi wameficha kila kitu kwahiyo tunazungumza kwa kile walichokizungumza, kama mkataba kweli umerekebishwa wautoe nje wauweke wazi wanaficha nini”, amehoji Mwabukusi.
Amesema kusudi la Sheria zilizotungwa ni kulinda raslimali za Taifa na kutopoka hadhi ya nchi tofauti na ambavyo sasa Tanzania imeingia mkataba na Dubai ambayo sio nchi kama sheria inavyoelekeza hivyo sheria na katiba zinakanyagwa.
“Mimi nadhani hata Magufuli (Hayati Dkt.John Magufuli) huko aliko maana ndiye aliyeleta hizi sheria mbili, nadhani hata mwili unashtuka yaani hawezi kuamini hawa aliowacha wanaweza kuitapikia ile sheria kwa namna wanavyofanya. Yaani nchini kumekuwa na udalali usiokuwa wa kawaida wa Ardhi, wa raslimali za asili yaani ndio viongozi wetu wako bize hapa hawana nguvu wala muda wa kushughulikia Katiba ukiwaambia kuhusu Katiba wanasema muda hautoshi ila kwenye kuuza mali za Tanganyika wepesi kuliko kipanga. Haya mambo ni hatari kwa nchi yetu na wa-Tanganyika tulione hili yaani sio la mtu tusikubali”, Ameeleza Wakili Mwabukusi.