Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kulifuatilia kwa karibu suala la mwanasiasa Tundu Lissu, lakini bila kuingilia mchakato wa kisheria unaoendelea mahakamani.
Ahadi hiyo imetolewa jana katika mazungumzo yake na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, yaliyofanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wakili Mwabukusi, baada ya kikao hicho, viongozi hao wawili walijadili masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya sheria na demokrasia, huku wakigusia pia nafasi ya wanasheria katika kulinda utawala wa sheria, kukuza demokrasia na kuhakikisha haki za wananchi zinasimamiwa ipasavyo.
Mwabukusi alisema alifika Ikulu kuwasilisha majumuisho ya mapendekezo ya wadau wa sheria na demokrasia, akisisitiza haja ya kuwepo mifumo thabiti ya uwajibikaji na uwazi.
Masuala yaliyoibuliwa
Miongoni mwa hoja zilizowasilishwa kwa Rais ni:
- Haki za ushiriki katika chaguzi – kuondoa vikwazo vya kiufundi vinavyoweza kunyima wananchi na wagombea haki ya kugombea au kushiriki katika uchaguzi.
- Changamoto za utekaji na kutoweka kwa watu – akieleza umuhimu wa kulinda haki za msingi za raia.
- Mageuzi ya mfumo wa uchaguzi – kuhakikisha chaguzi huru, haki na shirikishi bila hila au vizuizi visivyo halali.
“Nilihimiza mageuzi yatakayowezesha uchaguzi huru, wa haki na shirikishi, ili wananchi wapate viongozi wanaowataka kupitia sanduku la kura bila hila na bila kuondolewa wagombea au kuzuiwa kwa mawakala,” alisema Mwabukusi baada ya kikao hicho.
Msimamo wa Rais Samia
Rais Samia, kwa upande wake, alisema amepokea mapendekezo yote yaliyowasilishwa na ataangalia namna bora ya kuyatekeleza kulingana na mazingira na muda.
Alibainisha kuwa baadhi ya mapendekezo yanaweza kutekelezwa kwa muda mfupi, mengine kwa muda wa kati, na mengine yatahitaji muda mrefu. Aidha, alisisitiza kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha taifa linaingia kwenye uchaguzi ulio bora zaidi, ulio huru na wa haki kwa Watanzania wote.