Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwambukusi, amesema kuwa TLS siyo kikundi cha kigaidi bali ni taasisi halali inayofanya kazi kwa mujibu wa sheria, ikiwa na haki ya kuishauri, kupongeza, na hata kuikosoa serikali pale inapobidi.
Akizungumza leo jijini Dodoma katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika kwenye viwanja vya Chinangali, Mwambukusi amekanusha madai kuwa uongozi wa TLS umenyamazishwa na serikali.
“Kuna watu wanaodai kuwa tumenyamazishwa au ‘tumelamba asali’, lakini ukweli ni kwamba sisi siyo kikundi cha kigaidi. Tunafanya kazi kwa mujibu wa sheria, tukiwa na uhuru wa kushirikiana na yeyote. Kama serikali imefanya vizuri, tunao wajibu wa kuisifia; na pale inapokosea, tunapaswa kuikosoa kwa maslahi ya umma,” amesema Mwambukusi.
Kuhusu gari walilopewa na Serikali amesema gari hilo haikuwa na lengo la kuwaziba mdomo isipokuwa TLS inalitumia kwa kuwafikia watu na kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi waliopo ngazi ya chini kabisa.
“Mbona vyama vya siasa vina wabunge lakini bado vinapokea ruzuku kutoka serikalini? Leo hii kuna watu wanaopinga sisi kupewa gari, ilhali lengo letu ni kuwahudumia wananchi. Kila mtu mwenye nia njema anaweza kutusaidia ili tuendelee kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi,” ameongeza.
Kadhalika Mwabukusi amesema chama hicho kinaposhirikiana na Serikali haimaanishi kwamba wanalamba asali bali wanafanya kazi kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki yake.
“Tunapata changamoto watu wanapoona tukishirikiana na Serikali, wanafikiri tunalamba asali. TLS si kikundi cha magaidi, kwa hiyo sehemu ya kuonya tutaonya kwa haki, ya kupongeza tutapongeza kwa haki, ya kushiriki kufanya kazi tutashiriki pamoja, kulijenga Taifa letu na kumhudumia Mtanzania,” amesema Mwabukusi