Mwaka 2024 waelezwa kuwa mwaka hatari zaidi kwa wanawake wa Kenya

Karibu wanawake 200 wa Kenya waliuawa katika visa vya ukatili wa kijinsia mwaka 2024, ikiwa ni mara mbili ya idadi ya mwaka uliopita, kulingana na taarifa kutoka kwa vikundi vinavyofuatilia hali hiyo.

Tatizo la ukatili wa kijinsia limekuwa likikubalika kwa kiasi kikubwa nchini Kenya, ambayo ni mojawapo ya nchi za Afrika Mashariki. Wakati wa maandamano ya mwaka jana jijini Nairobi, wanaharakati walikabiliana na gesi ya machozi kutoka kwa polisi walipojaribu kuandamana kudai kumalizika kwa mauaji ya wanawake.

Ripoti ya pili ya mwaka ya Mradi wa Kimya cha Wanawake –– ushirikiano kati ya kampuni ya takwimu ya Odipo Dev na chombo cha habari cha Africa Uncensored ilibaini kwamba wanawake 170 waliuawa, kutoka 95 waliouawa mwaka uliopita.

“2024 ilikuwa mwaka hatari zaidi kwa wanawake wa Kenya, na kwa bahati mbaya, hakuna ishara ya hali hii kupungua,” alisema mtafiti mkuu, Patricia Andago.

Nairobi iliona idadi kubwa ya mauaji ya wanawake, ambapo vifo 28 viliripotiwa, kulingana na ripoti hii inayotokana na uchambuzi wa mauaji 930 ya wanawake tangu mwaka 2016, na kutumia ripoti za mahakama na vyombo vya habari.

Karibu asilimia 70 ya mauaji haya yalitekelezwa na wenzi wa karibu, na asilimia 61 yalifanyika katika maeneo ya kibinafsi au “nyumbani.”

“Wanawake wanahitaji kujisikia salama mahali popote walipo. Hivi sasa, wanakutana na hatari kubwa nyumbani,” alisema Felix Kiprono, mkuu wa vyombo vya habari katika Odipo Dev.

Wanawake vijana wenye umri wa miaka 18-35 walikuwa nusu ya wahasiriwa, huku wanaume wa kundi hili la umri wakihusishwa na asilimia 66 ya watuhumiwa.

Ripoti hii ilitolewa wiki moja baada ya kukamatwa kwa mwanaume mwenye umri wa miaka 29, aliyetambuliwa akiwa na mabaki ya mwili wa mwaname anayeaminika kuua mkewe  jijini Nairobi.

Mwaka jana, taifa lilishtuka na kifo cha kikatili cha mchezaji wa riadha kutoka Uganda, Rebecca Cheptegei, ambaye mchumba wake alimwaga petroli na kuwasha moto nyumbani kwake.

Mashirika ya haki za binadamu yamekuwa yakihamasisha elimu bora na adhabu kali kwa wahalifu.

Ripoti hiyo ilibaini kwamba viwango vya hukumu vimeongezeka kwa asilimia 118 kutoka mwaka uliopita, “kiwango cha juu zaidi tangu 2018,” huku hukumu ya wastani ikiendelea kupanda kwa miaka mitatu, hadi kufikia miaka 23.

Hata hivyo, haki ilikuwa inachelewa, huku kesi zikichukua wastani wa miaka minne kutoka kufunguliwa hadi kutoa hukumu, na visa vikizidi kuwa vikali, huku ongezeko la mashambulizi ya kingono likiwa ni asilimia 7 na ongezeko la visa vya “kuchinjwa” likiwa ni asilimia 6.