Mwana wa Museveni asema haamini uhuru wa vyombo vya habari, aagiza kufungwa kwa NTV na Daily Monitor

Mkuu wa Jeshi la Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ametangaza kufungwa kwa taasisi ya habari ya Nation Media Group (NMG), inayomiliki gazeti la Daily Monitor, kituo cha televisheni cha NTV Uganda pamoja na vituo kadhaa vya redio, akisema haamini katika uhuru wa vyombo vya habari.

Muhoozi, ambaye pia ni mtoto wa Rais Yoweri Museveni, alitoa agizo hilo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X siku ya Jumapili, akitangaza kuwa shughuli za NTV Uganda na gazeti la Daily Monitor zimesitishwa kuanzia siku hiyo.

“Nchini Uganda, siamini katika uhuru wa vyombo vya habari. Vyombo vya habari vinapaswa kuongozwa na makada wa mapinduzi,” aliandika Muhoozi kwenye ukurasa wake wa X.

Baada ya tangazo hilo, gazeti la Daily Monitor lilisema kupitia mtandao wa X kuwa makao yake makuu yaliyoko jijini Kampala yalikuwa yamezingirwa na wanajeshi wenye silaha, huku shughuli za kawaida zikisitishwa.

Mbali na NTV Uganda na Daily Monitor, hatua hiyo pia iliathiri vyombo vingine vinavyomilikiwa na Nation Media Group, ikiwemo Dembe FM, KFM, Spark TV na The East African.

Mwandishi mmoja mwandamizi wa NTV Uganda, ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema kuwa wanajeshi walivamia ofisi na studio za kituo hicho usiku wa kuamkia Jumapili na kuamuru wafanyakazi wote kuondoka.

“Tumefungiwa katika studio na ofisi za NTV. Hakuna mtu anayeruhusiwa kuingia wala kutoka. Wafanyakazi waliokuwa kazini usiku waliamriwa kuondoka mara moja,” alisema.

Katika taarifa yake, Nation Media Group ilisema operesheni hiyo ya kijeshi ilifanyika majira ya saa saba usiku kwa saa za Uganda, ambapo umeme ulikatwa na shughuli za kampuni hiyo kusimamishwa kwa muda.

Aidha, Muhoozi aliagiza polisi kumkamata Mkurugenzi Mtendaji wa Nation Media Group Uganda, Susan Nsibirwa, mara tu watakapomuona. Hata hivyo, baadaye alifuta agizo hilo akisema msemaji wa Serikali, Alan Kasujja, angechukua hatua zinazostahili kuhusu suala hilo.

Muhoozi aliishutumu Nation Media Group kwa kile alichokiita “miaka mingi ya kumkashifu”, akisisitiza kuwa hatua ya kufunga taasisi hiyo ya habari imeidhinishwa na Rais Yoweri Museveni, ambaye ameiongoza Uganda kwa takribani miaka 40.

Hatua hiyo imekuja wakati mashirika ya kutetea haki za binadamu na wanasiasa wa upinzani nchini Uganda wakikabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa mamlaka. Shirika la kutetea haki za binadamu la Agora limeitwa na polisi kujibu tuhuma za udanganyifu na utakatishaji fedha, huku mwanasheria Erias Lukwago, anayemtetea kiongozi wa upinzani Kizza Besigye, akiripotiwa kukamatwa na kushtakiwa kwa tuhuma zinazohusiana na uhaini.

Mashirika ya kimataifa ya kutetea uhuru wa vyombo vya habari yamekosoa hatua hiyo. Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari (CPJ) imesema matumizi ya vikosi vya usalama kutekeleza vitisho dhidi ya vyombo huru vya habari ni ishara ya kuzorota kwa uhuru wa habari nchini Uganda.

Kwa upande wake, shirika la kutetea haki za binadamu la Vocal Africa lenye makao yake nchini Kenya, limesema uvamizi huo ni jaribio la kunyamazisha vyombo vya habari huru na kudhoofisha nafasi ya kiraia katika ukanda wa Afrika Mashariki. Shirika hilo limetaka wanajeshi kuondolewa mara moja katika ofisi za Nation Media Group Uganda na kuruhusu vituo vyote vilivyoathiriwa kurejea hewani.

Hata hivyo, Muhoozi amesisitiza kuwa vyombo hivyo vya habari havitaruhusiwa kurejea kufanya kazi bila idhini yake.

“Kuanzia sasa vyombo vyote vya habari nchini Uganda vitafuata sheria. Nitawakamata watu wengi zaidi,” aliandika kupitia mtandao wa X.

Kwa mujibu wa ripoti ya Reporters Without Borders (RSF), Uganda inashika nafasi ya 143 kati ya nchi 180 duniani katika faharasa ya uhuru wa vyombo vya habari, hali inayoonyesha changamoto zinazoendelea kuhusu mazingira ya uandishi wa habari nchini humo.