Mwanafunzi ajinyonga kisa kutoipenda shule aliyokuwa akisoma

Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari Lumbira kata ya Luanda wilayani Mbozi mkoani Songwe,Japhari Mwashitete  (16) amekutwa amefariki dunia kwa kujinyonga darasani huku kukiwa na ujumbe wa sababu ya kujinyonga ukieleza kuikataa shule hiyo.

Kamanda wa polisi mkoani Songwe, Theopista Mallya amesema wamepokea taatifa za kuiinyonga mwanatunzi huyo juzi tarehe 3 Julai 2023 muda wa saa 10 jioni.

Amefafanua kuwa polisi walifanya taratibu za vipimo vya daktari na kubaini amekufa kwa kujinyonga hivyo polisi wakaamua kuruhusu familia kuendelea na taratibu za mazishi. 

Kamanda Malya amesema baada ya kifo hicho waliangalia kwenye mfuko wa suruali ya mwanafunzi huyo na kukuta karatasi yenye maandishi yenye ujumbe wa kukataa kusoma shule ya Lumbira na badala yake anataka kusoma shule ya Myovizi iliyopo kilometa chache kutoka shule hiyo

Amesema kufuatia tukio hilo hakuna mtu ama watu waliokamatwa wakihusishwa na tukio hilo huku jeshi lake likiendelea na uchunguzi wa kina kuona kama kuna mtu ama watu wamehusika na tukio hilo. 

Kufuatia tukio hilo wananchi wanaozunguka eneo hilo wamesikitishwa na kitendo cha mwanafunzi huyo kuchukua maamuzi hayo magumu huku wakitaka uchunguzi zaidi ufanyike kuona kama kuna mtu kahusika.