Mwanafunzi wa darasa la saba Johnson Thomas (14) aliyekuwa akisoma katika Shule ya Msingi Buhalahala mjini Geita nchini Tanzania, amekutwa amefariki dunia na mwili wake kutupwa pembeni ya mto karibu na Barabara ya Buhalahala kwenda Kijiji cha Nyakato.
Tukio la mtoto huyo kuuawa ni tukio la tatu ndani ya wiki mbili ambapo watoto wengine wawili mmoja akiwa na miaka miwili aliuawa kwa kukatwa shingo na mwingine wa miaka saba inadaiwa alilawitiwa na kubakwa kisha kukatwa shingo wilayani Nyang’hwale mkoani humo.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Henry Mwaibambe amesema tukio hilo limetokea Juni 18 saa 11 jioni katika Kijiji cha Buhalahala.
Amesema mtoto huyo alitoka nyumbani kwao Juni 12 kwa usafiri wa bajajaji akielekea Buhalahala kushona sare za shule na mara ya mwisho alionekana na mwanafunzi mwenzake akielekea barabara inayokwenda ofisi za GPH. Tangu siku hiyo hakurejea mpaka mwili wake ulipopatikana Juni 18.
Kamanda amesema mwili huo umekutwa na majeraha mguu wa kushoto kama ulipondwa na kitu kizito ambacho hakijafahamika.
Naye msemaji wa familia ya mtoto huyo, Theophil Mkwata amesema mwili huo umekutwa unyayo umekatwa na jicho kunyofolewa.
Kwa mujibu wa Kamanda uchunguzi uliofanyika umebaini unyayo ulikuwa umepondekapondeka na jicho kuumia.
Hadi sasa hakuna aliyekamatwa na polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.