Mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Lyoto jijini Mbeya, Ibrahim Edson (12 ) amefariki dunia baada ya kijinyonga ndani ya chumba alichokuwa akilala kwa kutumia kamba ya katani.
Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Benjamin Kuzaga amewaambia waandishi wa habari leo kuwa mwanafunzi huyo alifikia hatua ya kujitoa uhai baada ya kufokewa na wazazi wake.
Amesema kuwa tukio hilo lilitokea Februari 27, mwaka huu saa 2.00, ambapo marehemu alikutwa akiwa ananing’inia ndani ya chumba chake.
“Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha kuchukua jukumu la kujinyonga ni baada ya wazazi wake kumfokea na ndipo alichukua aumuzi huo mgumu wa kupoteza uhai wake,” amesema.
Kamanda Kuzaga amewataka wazazi na walezi kuwa makini na kuzungumza kwa ukaribu na watoto katika familia pindi inapojitokeza changamoto ili kuwepusha kujua majukumu magumu ya kujitoa uhai.
Mkazi wa jijini hapa, Subira Joel aliomba Serikali kupitia Wizara ya Elimu kuwepo kwa walimu au wataalamu wa saikolojia kuanzia elimu ya msingi, sekondari mpaka vyuo vikuu ili kudhibiti matukio yaliyoshamili kwa watu kuchukua hatua za kujikatisha uhai kutokana na kuwepo kwa msonga wa mawazo.
“Ukitaka kuangalia kipindi hiki watoto wanaojinyonga ni wadogo jambo ambalo linatafakarisha jamii na huwenda marehemu sababu ya kujinyonga isiwe ni kufokewa bali ni siri yake,” amesema.
Amesema kutokana na kuwepo kwa matukio ya watoto kuripotiwa kujinyonga Serikali ione haja ya kuwepo kwa wataalamu wa saikolojia ili kuweza kubaini watoto walio na changamoto na kukaa nao kuwaweka sawa kiakili.