Mwanasiasa mkongwe wa Uganda Miria Matembe aripotiwa kutekwa Kampala

Mwanasiasa mkongwe wa Uganda na mtetezi wa haki za wanawake, Miria Matembe, mwenye umri wa miaka 72, ameripotiwa kutekwa na watu wanaodhaniwa kuwa maofisa wa usalama baada ya kujificha kwa siku mbili kufuatia msako uliofanywa nyumbani kwake eneo la Luzira, jijini Kampala.

Taarifa hizo zimetolewa na mpwa wake, Junior Dave Kazoora, maarufu kama “Uncle JK”, ambaye amesema Matembe alichukuliwa na watu wanaoaminika kuwa maofisa wa polisi takribani saa mbili kabla ya kutoa taarifa hiyo.

“Kufikia saa mbili zilizopita, alichukuliwa na watu wanaoaminika kuwa maofisa wa polisi na kupelekwa Mbuya. Amepewa dawa zake. Kesho au Jumanne tutajua kama atapelekwa gereza la Luzira au ataachiliwa huru,” alisema Kazoora.

Awali ilidhaniwa kuwa Matembe alikamatwa siku ambayo vikosi vya usalama vilivamia nyumba yake mnamo Juni 26. Hata hivyo, Kazoora amesema mwanasiasa huyo alifanikiwa kukwepa kukamatwa baada ya kupewa taarifa za siri alipokuwa akifanya mazoezi ya kukimbia.

Kwa mujibu wa familia, Matembe alipokea taarifa kuhusu msako huo na kujificha katika eneo lenye miti karibu na nyumbani kwake kabla ya kupata hifadhi kwa jirani. Baadaye alihamia nyumbani kwa rafiki yake ambako aliendelea kujificha hadi alipokamatwa.

Kazoora amesema siku moja kabla ya tukio hilo alizungumza na baadhi ya maofisa waandamizi serikalini ambao walimhakikishia kuwa vyombo vya usalama havikuwa tena vinamtafuta Matembe na kwamba angeweza kutoka mafichoni bila hofu.

Hata hivyo, amesema baada ya kuwafahamisha wanafamilia na marafiki kuhusu taarifa hizo, vyombo vya usalama vilifanikiwa kufuatilia mawasiliano yao na kubaini mahali alikokuwa amejificha.

“Nilituma ujumbe kwa wanafamilia, lakini asubuhi walikamatwa marafiki wawili wa shangazi. Nafikiri walitumia simu za kawaida badala ya WhatsApp au Telegram, jambo lililorahisisha kufuatiliwa. Kupitia wao ndipo vyombo vya usalama vilipobaini alikokuwa Matembe,” alisema.

Mapema Jumatatu, marafiki wa Matembe, Dk. Sarah Bireete na Eunice Musiime, walikamatwa na maofisa wa usalama na kuzuiliwa kwa muda kabla ya kuachiwa huru.

Mume wa Matembe, Nehemiah Matembe, amesema maofisa wa usalama walivamia nyumba yao bila kujitambulisha wala kueleza sababu ya operesheni hiyo, kabla ya kuondoka bila kumkamata mtu yeyote.

Baadaye familia ilitangaza kutoweka kwa Matembe, ikieleza kuwa ilihofia huenda alikamatwa na maofisa wa usalama alipokuwa akifanya mazoezi ya kukimbia.

Miria Matembe ni Waziri wa zamani wa Maadili na Uadilifu nchini Uganda na mmoja wa waliohusika katika kuandaa Katiba ya Uganda ya mwaka 1995. Katika miaka ya karibuni amekuwa mmoja wa wakosoaji wakubwa wa Serikali ya Rais Yoweri Museveni, akilaani mara kwa mara madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu, kutoweka kwa watu kwa nguvu pamoja na kuongezeka kwa ushawishi wa jeshi katika masuala ya kisiasa.

Kazoora amesema familia ina matumaini kuwa ifikapo Jumanne itafahamu hatima ya Matembe.

“Tunaomba kila kitu kiwe sawa ifikapo Jumanne,” alisema.