Mwanasiasa wa Nigeria amekamatwa kwa madai ya utakatishaji fedha baada ya kukutwa na na $498,100 (£414,000) pesa taslimu siku moja kabla ya uchaguzi mkuu.
Dola hizo za kimarekani zilikutwa na polisi ndani ya gari la Chinyere Igwe. Bw Igwe, mwanachama wa chama cha upinzani cha PDP katika Baraza la Wawakilishi, pia alinaswa na orodha ya watu wa kuwapa pesa hizo, polisi wanasema.
Katika chaguzi zilizopita, wanasiasa wameshutumiwa kwa wizi wa kura kupitia ununuzi wa kura.
Nigeria imeunda upya sarafu yake, naira, kwa kiasi fulani ili kufanya iwe vigumu kwa wanasiasa kukusanya kiasi kikubwa cha fedha ili kuwahonga wapiga kura.
Hatahivyo, noti mpya hazitoshi, na kusababisha hasira na kufadhaika.
Watu wamekuwa wakipanga foleni kwa saa nyingi nje ya benki ili kupata pesa, mara nyingi bila mafanikio, huku wengine wakishambulia benki.
Asilimia 40 ya Wanigeria hawana akaunti za benki na hivyo wanategemea pesa taslimu kununua chakula, na kwa matumizi mengine ya kila siku.
Katika mtandao wa Twitter, polisi wa Jimbo la Rivers waliwataka “wagombea wote na vyama vya kisiasa kuzingatia vifungu vya Sheria ya Uchaguzi na sheria zingine muhimu”.
Uchaguzi huo unatabiriwa kuwa wenye ushindani mkubwa zaidi tangu kumalizika kwa utawala wa kijeshi mwaka 1999, huku wagombea watatu wote wakionekana kuchuana vikali.