Mwanaume mmoja nchini Tanzania akatwa sehemu za siri akiwa kwenye kilabu cha pombe

Mkazi wa Kijiji cha Orkine, wilayani Kiteto mkoani Manyara, Nanaa Mepukori (54) amelazwa katika hospitali ya wilaya hiyo baada ya kujeruhiwa kwa kukatwa sehemu zake za siri na watu wasiojulikana.

Mtoto wa mzee huyo, Leyaseki Mepugori (26) ameeleza kuwa alimkuta baba yake akiwa anavuja damu baada ya kufanyiwa ukatili huo.

“Nilimkuta mzee akiwa hoi, hajiwezi hata kidogo tulimpeleka zahanati lakini walitushauri kwenda hospitali ya Kiteto kwa matibabu ambapo mpaka sasa tunaendelea nayo hospitali ya Kiteto ingawa mpango uliopo sasa ni kumpeleka Dodoma kwa matibabu zaidi‚ÄĚ amesema mtoto huyo.

Tukio la mwanaume huyo kukatwa nyeti lilitokea Juni 28, 2022 usiku ambapo inadaiwa kuwa alikuwa kwenye kilabu cha pombe za kienyeji na alipotoka nje kujisaidia akakutana na watu hao na kumkata kwa kutumia kisu.

Mepugori amesema mara kadhaa amekuwa akisikia kauli za baadhi ya watu wakisema kuna wanaonunua viungo vya binadamu maarufu (kutoa vocha) hakuwa anaelewa lakini kilichotokea katika familia yake kinamfanya kuamini aliyokuwa anayasikia.

Mganga wa zamu hospitali ya Kuteto, Dk Achmedis Mpemba amethibitisha kumpokea mgonjwa huyo akisema alijeruhiwa kwa jaribio la kukatwa sehemu za siri na kusema kuwa kabla ya kufikishwa hapo hospitali alipelekwa zahanati moja wilayani humo na kuanza matibabu.

Hata hivyo, Dk Mpemba amesema mgonjwa huyo ilibidi ahamishiwe katika hospitali ya wilaya kupata matibabu zaidi baada ya kushonwa ingawa bado hali yake haijaimarika.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Benjamini Kuzaga amethibitisha kutokea tukio hilo na kuahidi taarifa baadaye juu ya tukio hilo.

Matukio watu kusaka viungo vya binadamu maarufu (vocha) yameendelea kusikika katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, ambapo hivi karibuni mwanamke mmoja aliuawa akiwa Kijiji cha Engusero akituhumiwa kusaka viungo hivyo.

Chanzo Mwananchi.