Mwanaume mmoja nchini Tanzania amemuua mkewe kwa kumkata sehemu za siri na kisha kumtoboa macho

Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linamshikilia mkazi wa Kijiji cha Ndinyika, Kata ya Karansi wilayani Siha, Stephano Sikawa (33), kwa tuhuma ya kumchinja hadi kumuua mkewe, Sioni Daudi (26), mbele ya mwanawe mwenye umri wa miaka minne.

Inadaiwa kuwa mtuhumiwa wa mauaji hayo ametekeleza unyama huo kwa kumkata sehemu zake za siri na kuchukua kiungo hicho, akakata viganja vya mkono wa kulia, vidole viwili na kumtoboa macho mwenzi wake huyo.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani humo, Kamishna Msaidizi Simon Maigwa, Sioni aliuawa na mumewe juzi akiwa nyumbani kwake kijijini huko.

“Ni kweli nimepokea taarifa kuhusu mauaji hayo ya kikatili. Mume wa marehemu imebidi tumkamate kwa sababu anahusishwa na mauaji hayo.

Kuna rekodi ya maneno yake aliyokuwa akiyasema huko nyuma kwamba atamfanya kitu kibaya.

“Alikuwa ni mtu na mpenzi wake na ni watu ambao walikuwa na wivu wa mapenzi. Sasa hivi Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa pamoja na Polisi Dawati la Jinsia la Wilaya na OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya) wako wanafuatilia sakata hilo,” alisema.

Alipotafutwa na Nipashe jana kuzungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Ndinyika, Joseph Laizer, alikiri mauaji kutokea usiku wa kuamkia juzi.

“Sisi wananchi tumefahamu kuhusu mauaji hayo majira ya saa 1:08 juzi usiku baada ya mtoto wa marehemu aitwaye… (anataja jina la mtoto mwenye umri wa miaka minne), kushuhudia mauaji na kutoka ndani. 

“Alituambia mama yake yuko… (alitamka neno lililomaanisha hakuwa na nguo) na amelala mlangoni. Hayo maneno alimwambia babu yake mdogo ambaye ni jirani kuwa mama yake amelala chini, akimwamsha haongei,” alisema.

Tukio hilo ni mwendelezo wa matukio mengi ya mauaji ya kikatili yanayoripotiwa nchini, mwanzoni mwa mwaka huu kukishuhudiwa matukio mengi ya aina hiyo.

Viongozi wa dini na wadau wa haki za binadamu, wakiwamo wabunge na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) wameshapaza sauti dhidi ya matukio hayo, wakitaka hatua zichukuliwe serikalini na jamii kwa ujumla kudhibiti hali hiyo.

CHANZO NIPASHE