Watu wanne wamefariki dunia papo hapo na wengine 36 kujeruhiwa baada ya basi la Kampuni ya Kilimanjaro walilokuwa wakisafiria kutoka Tunduma kwenda Dar es salaam, kupinduka na kutumbukia kwenye korongo katika eneo la Senjele wilayani Mbozi katika Mkoa wa Songwe wakati likijaribu kuyapita magari mengine.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe, Rashid Ngonyani amesema miili ya watu wawili kati ya wanne ndio imetambuliwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe ambapo ni Novatus Charles na Rashid Sadam wote wakazi wa Jiji la Dar es Saalam.
Kamanda Ngonyaji amesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa dereva wa basi la Kilimanjaro Express bwana Mjahidi Waziri (39) ambaye alikuwa akijaribu kuyapita magari mengine.
Amesema Waziri baada ya kutokea kwa ajali hiyo alijisalimisha kwa jeshi la Polisi ambapo hadi sasa anashikiliwa na baadae atafikishwa mahakamani.
“Ajali hii imetokea majira ya saa moja asubuhi eneo la Senjele ambapo dereva wa basi la Kilimanjaro alikuwa kwenye mwendokasi alikuwa akijaribu kuyapita malori ambapo uso kwa uso alikutana na lori lingine na kuamua kudumbukia korongoni,”alieleza Ngonyani.
Akizungumza katika eneo la ajali, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba amesema majeruhi wote 36 wanaendelea kupatiwa matibabu na kwamba kati yao wawili wamepewa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya MZRH