Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CHADEMA nchini Tanzania Hashim Issa Juma, mpaka sasa bado anashikiliwa na polisi katika kituo cha polisi Oysterbay, ambapo anatuhumiwa kuchapisha taarifa za uongo chini ya sheria ya Makosa ya Mtandao.
Oktoba 3 taarifa zilieza kuwa Mzee Hashimu alichukuliwa nyumbani kwake visiwani Zanzibar na watu waliojitambulisha kuwa ni askari na kwa mujibu wa familia yake watu hao hawakuwa wamevaa sare za polisi wala hawakuieleza familia hiyo kwamba wanampeleka wapi.
Hata hivyo Oktoba 4,2021, Katibu Mkuu wa chama cha CHADEMA , John Mnyika kupitia ukurasa wake wa Twitter aliandika kwa kusema kwamba mzee Hashimu amesafirishwa kutoka Zanzibar na kuletwa jijini Dar es salaam, na kuwaelekeza mawakili wa chama hicho kufungua kesi dhidi ya polisi.
Hata hivyo wadadisi wa mambo ya mlengwa wa kushoto wanasema huenda kukamatwa kwa mzee Hashimu si kwa kosa la kuchapisha taarifa za uongo pekee bali ni mbinu za polisi katika kudhibiti wale wote wanaozungumzia masuala ya Katiba Mpya.
Ikumbukwe Mzee Hashimu amekatwa siku mbili baada ya kuzungumza kwenye mkutano wa wanahabari kuhusu misimamo yao kama wazee wa chama hicho katika kudai Katiba Mpya na Tume huru ya uchaguzi, huku akiikosoa Serikali kwa namna ambavyo inaendesha nchi.
Katika moja ya nukuu alizonukuliwa mzee Hashimu wakati wa mkutano huo alisema kwamba
“”Rais tu hawezi kuwa na mfumo wa uchumi wa nchi na uchumi wa wananchi wake wote, mfumo huo haupo duniani kote, ndio maana tunadai katiba mpya ili kila Rais anayepatikana aongozwe na katiba hiyo na si kuja na mifumo yake binafsi katiba ambayo fedha za umma zitaogopwa” Hashim Issa
Kwa sasa chama CHADEMA, kimekubali kufa na kupona katika kile wanachodai watalinda maslahi ya umma kwa kudai haki itakayotokana na kupatikana kwa Katiba Mpya, madai ambayo hivi sasa yanaendelea kuwagharimu kwani mbali na Mwenyekiti wao Freeman Mbowe kusota mahabusu, kamatakamata inaendelea na hivi juzi tu wanachama wake kutoka Baraza la Wanawake CHADEMA waliingia mikononi mwa polisi wakiwa wanafanya mazoezi ya viungo.