Namibia yamchagua rais wake wa kwanza mwanamke

 Chama cha SWAPO cha nchini  Namibia kilitangazwa mshindi jana Jumanne katika uchaguzi wa wiki iliyopita uliojaa utata, na kuleta rais wa kwanza mwanamke katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika baada ya kura zilizokuwa na mgogoro ambao upinzani mkuu tayari umesema hautautambua.

Naibu Rais Netumbo Nandi-Ndaitwah alijipatia zaidi ya asilimia 57 ya kura, akifuatiwa na mgombea wa upinzani mkuu, Independent Patriots for Change (IPC), aliyejipatia asilimia 25.5, ilitangaza mamlaka ya uchaguzi.

Nandi-Ndaitwah, mwenye umri wa miaka 72, anakuwa rais wa kwanza mwanamke wa nchi hii tajiri kwa madini, ambayo imekuwa ikiongozwa na SWAPO tangu uhuru kutoka Afrika Kusini ya ubaguzi wa rangi mwaka 1990. 

Uchaguzi wa tarehe 27 Novemba ulikuwa kipimo cha uthabiti wa SWAPO katika madaraka kwa miaka 34, huku IPC ikipata umaarufu kutoka kwa vizazi vya vijana wanaojali zaidi kuhusu ukosefu wa ajira na usawa kuliko uaminifu kwa vyama vya wakati wa mapambano.

Upigaji kura uliongezwa hadi tarehe 30 Novemba baada ya migogoro ya uchaguzi  ikiwa ni pamoja na upungufu wa karatasi za kupigia kura, hali iliyosababisha foleni ndefu. Baadhi ya wapigakura walijitoa katika siku ya kwanza ya uchaguzi baada ya kusubiri hadi masaa 12.

IPC ilisema hili lilikuwa ni jaribio la makusudi la kuwachosha wapigakura na haito kubali matokeo.

Mgombea wao wa urais, Panduleni Itula, mwenye umri wa miaka 67, alisema wiki iliyopita kuwa kulikuwa na “kasoro nyingi.”

“IPC haitatambua matokeo ya uchaguzi huo,” alisema Jumamosi, siku ya mwisho ya kupiga kura iliyoongezwa. Chama hicho kinasema kitatumia “mchakato wa kisheria kufuta matokeo ya uchaguzi.”

Akijibu tangazo la ushindi la SWAPO, msemaji wa IPC, Imms Nashinge alisema chama hicho kinaendelea na msimamo wake.

Itula wiki iliyopita aliwataka wafuasi wa chama chake kubaki watulivu lakini pia kusimama imara kupigani haki yao ya kidemokrasia. 

Shirika la wahanga wa haki za binadamu la Afrika ya Kusini linalofanya kazi kama waangalizi wa uchaguzi, lilisema pia kwamba ucheleweshaji katika upigaji kura ulilenga kwa makusudi na ulikuwapo kwa kiwango kikubwa.

  • Uzembe –
 Tume ya Uchaguzi ya Namibia (ECN) ilikubali makosa katika utayarishaji wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na upungufu wa karatasi za kupigia kura na joto kupita kiasi kwa vifaa vya kielektroniki vilivyotumika kuorodhesha wapiga kura.

Kati ya wapiga kura milioni 1.5 waliosajiliwa katika nchi hii yenye idadi ndogo ya watu, karibu asilimia 77 walijitokeza kupiga kura kwenye uchaguzi wa rais. 

“Wanajamii wa Namibia, uchaguzi ni ushindani kwa asili, lakini demokrasia inatufundisha kuungana mara baada ya kupiga kura. Ninawahimiza wananamibia wote kukubaliana na matokeo kwa roho ya umoja, utofauti, uelewa na upatanishi,” alisema mwenyekiti wa ECN, Elsie Nghikembua alipotangaza matokeo.

SWAPO pia ilikamata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Bunge la Kitaifa, ikishinda viti 51 ikilinganishwa na 20 za IPC. Idadi ya viti ya SWAPO ilikuwa chini ikilinganishwa na viti 63 walivyoshinda katika bunge la awali.

Uchaguzi huu ulionekana kuwa kipimo muhimu kwa SWAPO baada ya vyama vingine vya mapambano ya uhuru katika kanda hiyo kupoteza umaarufu miongoni mwa wapiga kura vijana, ikiwa ni pamoja na Chama cha Demokrasia cha Botswana kilichotimuliwa madarakani mwezi uliopita baada ya takriban miongo sita.

Namibia ni mzalishaji mkuu wa uranium na almasi, lakini wachambuzi wanasema si wengi miongoni mwa watu wake milioni tatu waliopata manufaa kutoka kwa utajiri huo kwa njia ya miundombinu bora na fursa za ajira.

Ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana wa umri wa miaka 15 hadi 34 unakadiriwa kuwa asilimia 46, kulingana na takwimu rasmi za mwaka 2018, ambayo ni karibu mara tatu ya wastani wa kitaifa.

Nandi-Ndaitwah, ambaye ni miongoni mwa wanawake wachache wanaoongoza barani Afrika, ni kiongozi mwenye ushawishi mkubwa katika SWAPO.

Mwanamke huyu mwenye sura inayojulikana kwa miwani yake ya dhahabu, alikubali kuwa naibu rais mwezi Februari mwaka huu. Alijitahidi kuonyesha hekima yake katika kampeni, ambapo mara nyingi alivalia buluu, nyekundu na kijani, rangi za chama chake na za bendera ya taifa.

Miongoni mwa ahadi zake za uchaguzi, Nandi-Ndaitwah alisema anatarajia “kutoa ajira kwa kuvutia uwekezaji kwa kutumia diplomasia ya kiuchumi.”