Aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amejiondoa kwenye utumiaji wa Mtandao wa X(Twitter) baada ya muda mfupi wa yeye uteuzi wake kama Waziri wa Habari kutenguliwa jana na Rais Samia Suluhu amabye amefanya mabadiliko madogo kwenye baraza lake la mawaziri.
Itakumbukwa kuwa taarifa ya Ikulu ya utenguzi wa Nape ilimkuta Waziri huyo wa zamani akiwa katikati ya hafla ya utoaji tuzo za wanawake wa kidigitali zilizofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam ambako alikuwa mgeni rasmi. Shughuli hiyo ilikuwa ikirushwa mubashara na kituo cha televisheni cha TV E. iliyotumwa kati ya majira ya saa mbili usiku na saa tatu.
Hii si mara ya kwanza kwa mwanasiasa huyo kupatwa na tenguzi ya aina hiyo kwani itakumbukwa kuwa katika mazingira yanayofanana, aliwahi kuondolewa katika Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo akiwa katika harakati za kupokea ripoti ya kamati aliyoiunda ya kuchunguzi tukio la uvamizi wa kituo cha redio cha Clouds mwaka 2018.
Nape aliteuliwa kushika kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari mwaka 2022, chini ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Amedumu ndani ya wizara hiyo kwa miaka miwili pekee na jana usiku wa Julai 21, 2024 aliondolewa bila kuelezwa sababu yoyote.
Hata hivyo kuondolewa kwake wakati huu kunahusishwa na kauli aliyotoa hivi karibuni iliyoibua mijadala katika mitandao ya kijamii, kuhusu ushindi wa uchaguzi nje ya boksi la kura.
Kauli hiyo iliyoibua mjadala mzito aliitoa Julai 15, 2024 usiku alipotembelea soko la Kashai mkoani Kagera na kuzungumza na wananchi.
Muktadha wa kauli hiyo ilikuwa ni kuwahakikishia ushindi wa Mbunge wa Bukoba Mjini, Stephen Byabato katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2025,
“Unajua nyie sikilizeni, matokeo ya kura sio lazima yawe ya kwenye boksi, inategemea nani anahesabu na kutangaza. Na kuna mbinu nyingi kuna halali, nusu halali na kuna haramu na zote zinaweza kutumika ilimradi mkishamaliza unamwambia Mwenyezi Mungu nisamehe,” alisema Nape Julai 15, 2024, akiwa mkoani Kagera.
Hata hivyo kujiondoa kwake katika mtandao wa X kumeibua maswali mengi kwa wadau hasa wanaomfatilia ambapo hadi sasa hajaweka wazi sababu za yeye kujiondoa katiaka mtandao huo ambapo ana wafatiliaji takribani milioni moja.