Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Tanzania, Nape Nnauye amewaomba radhi wananchi na wapenda demokrasia nchini kutokana na kauli aliyoitoa kuwa si lazima CCM ishinde kura halali za kwenye boksi, bali kuna njia nyingine za haramu zinazoweza kuifanya CCM ishinde.
Nape ameomba radhi leo ikiwa tayari kumekuwa na gumzo na sintofahamu iliyojaa mjadala wenye hisia mseto kufuatia kauli yake hiyo iliyozagaa mitandaoni tangu Julai 15,2024.
Kupitia Video aliyerekodi Nape amesema “Nimeuona mjadala kwenye mitandao, lakini kama nilivyosema kauli ile ilikuwa utani lakini naona umekuwa mjadala mrefu wakati huu kwa sababu tunaelekea katikia uchaguzi. Nawapa pole ambao wamesumbuliwa na kuteseka na huu mjadala, nawapa pole na naomba radhi, nasisitiza haikuwa serious,”amesema Nape.
Nape ambaye amewahi kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, alitoa kauli hiyo akiwa katika soko la Kashai mkoani Kagera na kuzungumza na wananchi wakati wa ziara yake mkoani humo.
Mwanasiasa huyo mashuhuri aliyeshika nyadhfa mbalimbali Serikalini na kwa sasa ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, amekua na kauli tata zinazoibua wengi wanaomtazama kama ni mtu ayedhihirisha kwamba Serikali anayoitumikia mara zote imekuwa ikitumia ubabe katika kufanikisha ushindi dhidi ya Wapinzani wao.
Kauli yake aliyoitoa Julai 15,2024 huko Kagera ilikuwa ina lengo la kumnadi mbunge mwenzake wa jimbo la Bukoba Mjini, Stephen Byabato katika kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.
Amenukuliwa akisema “Unajua nyie sikilizeni, matokeo ya kura sio lazima yawe ya kwenye boksi, inategemea nani anahesabu na kutangaza. Na kuna mbinu nyingi kuna halali, nusu halali na kuna haramu na zote zinaweza kutumika ilimradi tu mkishamaliza, unamwambia Mwenyezi Mungu nisamehe pale nilipokosea,” alisema.
Baada ya kuonekana kusambaa sana kauli hiyo na kuibua hisia mseto, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla alimkana Nape akisema kauli hiyo haitokani na msimamo wa chama hicho.
“Kuna kiongozi nimemsikia huko mitandaoni anasema eti ushindi wa uchaguzi hautokani na kura za kwenye boksi, mimi nataka niwaembie hiyo kauli isitazamwe kuwa inatokana na CCM,” alisema Makalla.
Hii si mara ya kwanza kwa Nape kutoa kauli tata zenye kuzua mjadala katika kipindi cha kuelekea uchaguzi, hata Juni 2015, akiwa ziarani Sengerema alisema “CCM ingeshinda uchaguzi mwaka huo hata kwa bao la mkono.”
Haya yanajiri wakati ambapo nchi inajiandaa na chaguzi za Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika 2025.