Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Tanzania Nape Nnauye ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukusanya kodi kwa kutumia taaluma na sio kutumia nguvu.
Nape ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utoaji tuzo kwa walipa kodi bora mwaka 2021/2022.
āWengi walisema tukifunga vikosi kazi ātask forceā hatutafaulu ukusanyaji wa mapato, lakini hapa nawatangazia tumeweza kukusanya kodi bila kutumia nguvu.ā amesema Waziri Nape
Amesema serikali ya awamu ya sita imekuwa sikivu na itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara wanaolipa kodi kwa hiari bila shuruti na itahakikisha inapunguza changamoto wanazokabiliana nazo.
āTabia ya vitisho kwa wafanyabishara si sawa, na hii tabia inafanywa na watu wa TRA wadogo wadogo, sasa hawa wadogo wadogo wasipake matope kazi nzuri inayofanywa na TRA na tuzo hizi zitaongeza hamasa kwa wengine kulipa kodi kwa uaminifu na kwa wakati.ā amesema Waziri Nape
Ameiagiza TRA kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kutoa elimu kwa wafanyabiashara juu ya fursa za uwekezaji nchini.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA Alphayo Kidata amesema, utoaji wa tuzo hizo umezingatia mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja utunzaji wa kumbukumbu za mlipa kodi, ulipaji kodi kwa hiari na kwa wakati pamoja na ushirikiano mzuri wakati wa ukusanyaji wa kodi.