Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Tanzania,Nape Nnauye amesema uchumi wa kidijitali utafikiwa endapo kutakuwa na miundombinu wezeshi kama ilivyo kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Mfumo wa Anwani za Makazi.
Nape ameyasema hayo leo mjini Dodoma, katika kikao kazi cha Wakuu wa Mikoa kuhusu kufanikisha utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi nchini humo ifikapo mwezi Mei mwaka huu.
Amesema kwa upande wa Mkongo serikali imefikia asilimia 55 ya lengo la 2025 ambapo zimejengwa kilomita 8,300 kati ya kilomita 15,000 zitakazotimiza lengo la kila mwananchi kupata intaneti ya kasi, huku upande wa Anwani za Makazi ilipangwa kufikia 2025 jumla ya kata 4067 ziwe zimewekewa miundombinu ya anwani za makazi.
Kwa mujibu wa Waziri Nape, hadi sasa utekelezaji umefanyika katika kata 135 ambayo ni sawa na asilimia tatu tu na kukiri kuwa kasi ndogo ndio iliopelekea uamuzi wa kubadili mkakati wa utekelezaji.
Amesema manufaa makubwa yatakayopatikana katika kufanikisha anuani ya makazi mwezi Mei mwaka huu, utakuwa na tija katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika Mwezi Agosti, 2022.
Aidha Nape, amesema tayari Wizara imejenga uwezo kwa watendaji na wataalamu wa Mikoa na Halmashauri zote nchini (196 za Tanzania Bara na Zanzibar) kuhusu utekelezaji na Matumizi ya Programu Tumizi ya Mfumo.
Wataalam hao watawajengea uwezo watendaji wa Vijiji/Mitaa ambao watatumika katika kukusanya taarifa za Anwani za Makazi na kutoa Anwani husika kwa Wananchi.
“Ili kutekeleza hili, tumeandaa Mwongozo ili kurahisisha utekelezaji katika Halmashauri. Aidha, kupitia bajeti ya Wizara yangu ya mwaka 2021/22 tulitengewa kiasi cha shilingi Bilioni 45 hata hivyo hadi kufikia mwezi Februari Wizara imepokea kiasi cha shilingi Bilioni 13,274,770,613.00 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi.” amesema Waziri huyo
Amesema kiasi cha shilingi bilioni 28 zitagawanywa katika mikoa yote Bara na Zanzibar kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji kwa haraka na tija.