Anaandika Ndolezi Petro
Hili la kugawa majimbo ni jambo la msingi sana kujadiliwa kwa mapana yake, na hoja yangu katika mjadala huu itajikita kuunga mkono ugawaji wa majimbo kwa kuangazia kiini cha mjadala wa kugawa majimbo ya uchaguzi kwa kuzingatia vigezo muhimu kwa maslahi ya wananchi.
Napingana na wale wote ambao hawaoni tija ya kugawa majimbo na wenye fikra za kuona hakuna maana yeyote, kundi la mtizamo huu wengi wao wanaweza kuwa hawana elimu juu ya umuhimu wa ugawaji wa majimbo na inawezekana hawafahamu jiografia ya majimbo ya vijijini.
Naungana na hoja ya kwamba ugawaji wa majimbo haupaswi kuwa suala la maslahi binafsi au kisiasa bali unatakiwa kuzingatia vigezo vya msingi kama idadi ya watu, jiografia, upatikanaji wa huduma za kijamii, na uchocheaji wa maendeleo ya kiuchumi.
Katika mjadala huu, kuna hoja mbili zinazokinzana: moja ikisema kuwa kugawa majimbo zaidi ni mzigo wa kiuchumi kwa taifa, na nyingine ikisema kuwa ni njia bora ya kusogeza huduma karibu kwa wananchi na kuboresha uwakilishi wa kidemokrasia.
Uhalisia ni kwamba iwapo ugawaji huu utaongozwa na tafiti makini na takwimu sahihi, basi utasaidia kuleta maendeleo badala ya kuwa mzigo kwa taifa.
Changamoto kubwa ni kuhakikisha kuwa mchakato huu hauchukuliwi kama nyenzo ya kisiasa bali kama mpango wa kimkakati wa maendeleo ya watu yenye uwakilishi wenye uwiano.
Ikumbukwe pia mchakato wa ugawaji wa majimbo ni mchakato wa kikatiba si takwa la mtu na katika hili Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inatambua mamlaka ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) amabayo kwa sasa inatambulika na sheria namba 2 ya mwaka 2024 kama Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) katika kupitia na kugawa majimbo ya uchaguzi.
-Vifungu vinavyohusiana na mamlaka hii ni kama ifuatavyo:-
Ibara ya 74(6) – Inatoa mamlaka kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kufanya marekebisho ya majimbo ya uchaguzi kwa kuzingatia vigezo mbalimbali vinavyohusiana na idadi ya watu, jiografia, na maendeleo ya eneo husika.
Ibara ya 75(1) – Inaeleza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaweza kufanya mapitio ya mipaka ya majimbo ya uchaguzi na kuyagawa upya kila baada ya muda fulani kwa kuzingatia mabadiliko ya idadi ya watu na mahitaji ya maendeleo.
Ibara ya 76 – Inasisitiza kuwa Tume inapaswa kuzingatia usawa wa uwakilishi na kuhakikisha kuwa mgawanyo wa majimbo unazingatia vigezo vya msingi ili kutimiza lengo la uwakilishi wa haki.
-TUSIRUDIE MAKOSA YA KUGAWA MAJIMBO KISIASA, TWENDE KWENYE MSINGI WA KISHERIA NA HOJA ZA KUWASAIDIA WANANCHI-
Katika hili natoa wito kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kwamba tukipitia takwimu za majimbo yaliyopo 214 ya Tanganyika (Tanzania bara) unakuta hakuna mgawanyo wa majimbo uliozingatia uwiono wa uwakilishi kwa sehemu kubwa uwakilishi umeachana sehemu kubwa sana na ifuatayo ni mifano
1)Kwenye Mkoa wa Kigoma kuna majimbo 8 ya uchaguzi huku ukiwa na jumla ya watu 2,470,967, Jiografia yake ikiwa na Takriban 45,066 km² ukilinganisha na Mkoa wa Mtwara una jumla ya Watu 1,634,947 na jiografia yake ikiwa ni Takriban 16,710 km² lakini Mkoa wa Mtwara una majimbo mengi kuliko Kigoma ambapo una majimbo 10 ya uchaguzi. Jiografia ya Mkoa mzima wa Mtwara wenye kilomita za mraba 16,710 inazidiwa na Wilaya Moja tu ya Mkoa wa Kigoma, Wilaya ya Uvinza yenye jimbo moja la uchaguzi Jimbo la Kigoma Kusini ambapo ina kilomita za mraba 28,901. Lakini pia katika Mkoa huu wa Mtwara kwenye Wilaya ya Masasi kuna majimbo matatu ya uchaguzi ambayo ni Lulindi, Masasi na Ndanda huku Wilaya nzima ikiwa na watu 314,778 lakini Jimbo la Kigoma Kusini lenye wakazi 458,353 na jiografia kubwa kuliko Mkoa mzima wa Mtwara ni Jimbo moja la uchaguzi hapa hakuna uwiano sawa kiuwakilishi uliozingatiwa. Kuna haja ya kugawa Jimbo la Kigoma Kusini na Jimbo la Kasulu Vijijini lenye wakazi 537,767.
2)Kwa Mkoa wa Tanga niagazie Jimbo la Pangani lina wakazi 75,645 lakini linamuwakilishi Bungeni huku katika Jimbo la Uchaguzi la Muhambwe Kigoma kuna Kata inaitwa Murungu ina wakazi 84,449 yenyewe inamuwakilishi Diwani yani uzito wa Uwakilishi wa Mbunge wa Jimbo la Pangani anazidiwa na Diwani wa Kata ya Murungu. Hapa hakuana uwiano wa uwakilishi uliozingatiwa
3)Kwa Mkoa wa Ruvuma niangazie Jimbo la Uchaguzi la Madaba ambalo lina wakazi 65,215 lina muwakilishi Bungeni sawa na Jimbo la Bariadi lenye wakazi 644,312. Hapa hakuna uwiano sawa wa uwkilishi wa wananchi kwa upande wa bariadi jimbo linalopaswa kugawanywa
4)Kwa upande wa Majimbo ya Mjini tuangazie Jimbo la Lindi Mjini lenye wakazi 95,098 linauwakilishi Bungeni sawa na Jimbo la Dodoma Mjini lenye wakazi 765,179. Hapa hakuna uwiano uliozingatiwa wa kiuwakilishi.
Mifano ni mingi sana hiyo ni baadhi tu kuonyesha kwamba ugawaji uliowahi kufanyika hakuzingatia vigezo vilivyowekwa kikatiba na sheria zetu na hapo ndipo najenga hoja kwamba mgawanyo uliendeshwa kisiasa. Sasa tunayo nafasi ya kurekebisha na kuwatendea haki wananchi wengine, haki ya kupata uwakilishi wenye uwiano sawa bila kuendeshwa kisiasa.
NINI KIFANYIKE WAKATI HUU WA MCHAKATO WA UGAWAJI WA MAJIMBO?
Kwanza lazima tuhakikishe kuwa ugawaji wa majimbo unazingatia usawa na haki kwa wananchi wote, yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa:
01.Tafiti na Takwimu Sahihi, Serikali na INEC zinapaswa kutumia takwimu rasmi kutoka kwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ili kuhakikisha kuwa ugawaji wa majimbo unafanyika kwa misingi ya idadi ya watu, jiografia, na mahitaji ya maendeleo. Kuondoa Ushawishi wa Kisiasa.
02.Ugawaji wa majimbo usifanywe kwa maslahi ya chama cha siasa cha CCM au wanasiasa binafsi wa CCM. Badala yake, mchakato uwe wa kitaalamu na wa uwazi kwa kuzingatia maslahi ya wananchi. Ushirikishwaji wa Wananchi na uwazi ni muhimu katika hili.
03.INEC inapaswa kuhakikisha kuwa mchakato wote unazingatia Ibara za Katiba zilizopo, hususan 74(6), 75(1), na 76, ili kuhakikisha haki na uwiano wenye usawa wa uwakilishi.
-MWISHO-
Ugawaji wa majimbo ya uchaguzi ni suala la msingi linalopaswa kufanywa kwa uwazi na kwa kuzingatia maslahi ya wananchi. Kwa sasa, kuna ushahidi wa wazi kuwa mgawanyo wa majimbo uliowahi kufanyika haukuzingatia vigezo vya idadi ya watu na jiografia, jambo linalosababisha uwakilishi usio na uwiano wenye usawa. Tukishindwa kufanya hivyo, tutakuwa tunarudia makosa ya nyuma ambayo yanazidi kuongeza ukosefu wa haki kwa wananchi wengi kupata uwakilishi wenye tija ya kuchochea maendeleo katika maeneo yao.
Andiko hili limeandikwa na Ndolezi Petro, Waziri Kivuli Ofisi ya Waziri Mkuu-Bunge, Sera , Vijana, Kazi na Ajira ACT Wazalendo.