
Serikali kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeanza kutekeleza tafiti mbalimbali zenye lengo la kukusanya taarifa muhimu kuhusu shughuli za biashara katika sekta rasmi na isiyo rasmi, pamoja na uzalishaji viwandani nchini.
Akizungumza jijini Dodoma, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk. Amina Msengwa, amesema tafiti hizo zinalenga kupata takwimu sahihi kuhusu uzalishaji, ajira, uwekezaji na mazingira ya biashara, ili kufuatilia mwenendo wa ukuaji wa biashara na viwanda.
Amefafanua kuwa taarifa zitakazokusanywa zitakuwa nyenzo muhimu kwa serikali na wadau mbalimbali, ikiwemo sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na watafiti, katika kubuni mikakati na programu zitakazoboreshha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
Aidha, Dk. Msengwa amesema utafiti wa Huduma za Fedha kwa Wafanyabiashara (Finscope MSME) utasaidia kutoa takwimu muhimu kuhusu upatikanaji wa huduma za kifedha, zikiwemo mikopo, akiba, bima pamoja na huduma za fedha za kidijitali kwa biashara ndogo sana, ndogo na za kati.
Ameongeza kuwa matokeo ya tafiti hizo yatatumika pia kupima maendeleo ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Ujumuishaji wa Kifedha Awamu ya Tatu pamoja na Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha.
Kwa upande wa sekta ya viwanda, utafiti maalum utafanyika ili kukusanya taarifa kuhusu orodha ya viwanda vilivyopo katika mikoa mbalimbali, aina ya bidhaa zinazozalishwa, idadi ya wafanyakazi, gharama za uzalishaji pamoja na mapato ya viwanda.
Taarifa nyingine zitakazokusanywa ni pamoja na masoko, matumizi ya teknolojia ya mitambo, usimamizi wa mazingira, mipango ya uwekezaji na changamoto zinazoikabili sekta ya viwanda nchini.
Kwa mujibu wa Dk. Msengwa, tafiti hizo zitafanyika katika maeneo 1,518 kote nchini, zikihusisha biashara na taasisi 8,624 pamoja na viwanda 4,245 vinavyotarajiwa kushiriki katika zoezi hilo muhimu la kitaifa.