Ndugu wa Sabaya wataka Rais Samia aingilie kati kesi ya Sabaya na wenzake, wataka Serikali ikumbuke mazuri aliyoyafanya Sabaya akiwa kiongozi

Mawakili wa upande wa utetezi kwenye kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wanne wameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kuahirisha kesi hiyo ili Sabaya apelekwe hospitali kutibiwa kutokana na uvimbe alionao kichwani.

Akitoa ombi hilo leo Juni 7, 2022 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Salome Mshasha, Wakili Hellen Mahuna amesema mshitakiwa namba moja ambaye ni Sabaya ni mgonjwa hivyo anapaswa kwenda kufanyiwa upasuaji.

“Mshitakiwa namba moja ni mgonjwa kutokana na uvimbe uliopo kichwani alioupata akiwa kazini, hivyo tunaomba kesi hii iahirishwe ili akafanyiwe upasuaji,” amesema Wakili Mahuna

Wakili wa upande wa mashtaka,Verediana Mlenzi ameileza mahakama hiyo kuwa upelelezi bado haujakamilika na kuiomba mahakama hiyo tarehe nyingine kwa ajili ya kesi hiyo kutajwa.

Hata hivyo hakimu Mshasha amewataka upande wa mashitaka kutekeleza na kuzingatia kauli yao ya mara ya mwisho waliyoieleza mahakamani Juni Mosi kuwa upelelezi umekamilika.

Mahakama hiyo imeiahirisha kesi hiyo hadi Juni 20 mwaka huu.

Nje ya Mahakama mara badaa ya shauri hilo kuahirishwa, Wanawake jamii ya kimasai kutoka Wilaya ya Hai pamoja na ndugu wa Sabaya wamemwomba Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati kesi hiyo

Wakiangua vilio huku wakiwa wameshika majani ya masala nje ya mahakama hiyo, wamemuomba Rais Samia ayakumbuke mazuri aliyofanya Sabaya wakati akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai.

“Ninaomba kwa unyenyekevu mkubwa tunajua mwenye mamlaka ni wewe Rais wetu mama Samia tunaomba kwa huruma yako ya umama tunajua Sabaya amefanya kazi nyingi akiwa serikalini, tunaomba utekeleze neno moja tuu la huruma tunajua kama ni kufundishwa amefundishwa tunaomba huruma yako mama Samia kwa ajili ya hawa watoto” amesema mwanamke mmoja aliyetambulika kwa jina la Anna Msuya huku akitokwa na machozi

“Serikali ya Tanzania tunaomba ituhurumie tunaomba uingilie kati mama,” amesema mwanamke hyo akiwa amepiga magoji pamoja na wanawake wengine nje ya mahakama

Ole Sabaya na wenzake, ambao ni Sylvester Nyegu, John Aweyo, Nathan Msuya na Antoro Assey, wanakabiliwa na mashtaka mapya saba, ikiwamo kuongeza genge la uhalifu, utakatishaji wa fedha, vitendo vya kuomba na kupokea rushwa pamoja ukiukwaji wa maadili ya kiutumishi.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, kosa la kwanza katika kesi hiyo ambalo linawahusu washtakiwa wote ni la kuongoza na kushiriki genge la uhalifu katika Wilaya ya Hai, Februari 2, mwaka jana.

Shtaka la pili, linamkabili mshtakiwa wa kwanza, Lengai Ole Sabaya, ambalo anadaiwa kulifanya Februari 22, mwaka jana, kwa kuomba rushwa ya milioni 30 kutoka kwa Godbless Swai katika eneo la Bomangombe, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.

Katika shtaka la tatu, Ole Sabaya peke yake, anadaiwa kujipatia rushwa ya milioni 30 kutoka kwa Elibariki Swai, kwa nia ya kuzuia taarifa za uchunguzi zilizohusiana na ukwepaji wa kodi.

Wakati shtaka la nne na la tano, linawakabili mshtakiwa wa pili, tatu, nne na tano, ambalo ni kumsaidia mshtakiwa wa kwanza (Ole Sabaya), kushawishi na kujipatia manufaa asiyostahili ya Sh. milioni 30 kutoka kwa Alex Swai, huku akijua ni kinyume na sheria.

Shtaka la sita linamkabili mshtakiwa wa kwanza (Ole Sabaya), ambalo ni ukiukwaji wa maadili ya utumishi, akiwa ni mtumishi wa umma katika Wilaya ya Hai, na shtaka la saba ni utakatishaji wa fedha, ambalo linawakabili washtakiwa wote.