Search
Close this search box.
Africa

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), zimesema changamoto zinazotokea wakati uchaguzi asilimia kubwa zinachangiwa na wasimamizi wa uchaguzi katika halmashauri, kata na vyama vya siasa na sio kwamba taasisi hizo hazipo huru.

Aidha, NEC na ZEC zimesema zipo tayari kupokea mabadiliko ya kisheria ambayo yatapendekezwa katika kuzifanya taasisi hizo kuepushwa na  malalamiko. 

Akizungumza na vyombo vya habari juu ya nini kiliwasilishwa na wakurugenzi wa NEC na ZEC ambao waligoma kuzungumza na waandishi wa habari, Kaimu Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Rais Samia Suluhu Hassan, Hamad Rashid amesema Mkurugenzi wa ZEC Khamis Kona Khamis amesema wao kama watumishi wa Serikali wamekuwa wakitekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Katiba, Sheria na kanuni na kwamba sio jibu la kuwa hawapo huru.

Mkurugenzi huyo amesema changamoto zinazotokea sio maelekezo ya ZEC bali baadhi ya watumishi ambao wanaamua kufanya kazi kwa utashi wao wa kivyama.

Amesema kuhusu utaratibu wa kuwepo siku mbili za kupiga kura Zanzibar ambapo maofisa wa vyombo vya usalama wanatangualia na kesho yake raia, ZEC waliwajibu kuwa kinachofanyika ni kwa mujibu wa sheria na kwamba iwapo kutatokea mabadiliko wao watatekeleza.

“Kimsingi ZEC wamesisitiza kuwa hakuna msukumo wowote wanaopata kuhusu uchaguzi na kwamba mapungufu ambayo yanafanyika wakati wa uchaguzi ni kutokana na baadhi ya watu kuamua kuegemea upande na sio sheria,” amesema.

Kaimu Mwenyekiti huyo amesema upande wa NEC ambao uliwasilisha maoni yao kupitia Mkurugenzi wa Uchaguzi, Dk. Wilson Mahera walisema malalamiko dhidi ya tume hiyo hayana mashiko kwa kuwa wao hawajawahi kuelekeza nini kifanyike katika chaguzi.

Amesema kwa upande wa NEC walienda mbali na kuainisha kuwa Katiba na Sheria inaruhusu makamishna kupendekezwa na kuwataka wadau kufanya hivyo ili Rais anavyotaka kuteua atoe katika hao.

“Ametuambia yeye kwa miaka mitatu ya uwepo wake NEC hajawahi kupigiwa simu au kupewa maelekezo nini kifanyike, hofu yao ni kwa wasimamizi wa uchaguzi ngazi za chini kutumia nafasi zao vibaya, lakini pia akavitaka vyama na wagombea kutoamini katika kushindwa,” amesema.

Amesema taarifa zinaonesha kuwa wale ambao wanashinda uchaguzi wawe chama tawala au upinzani hakuna malalamiko dhidi ya tume, ila tatizo kubwa ni pale ambapo mgombea anashindwa.

Hamad amesema NEC na ZEC wamesisitiza kila mdau kuheshimu Sheria, Katiba na kanuni kwa kuwa ndio muongozo wa uchaguzi.

Mwenyekiti huyo amesema viongozi hao walisema iwapo watumishi wa umma watajitenganisha na siasa ni dhahiri kuwa uchaguzi utakuwa wa haki na huru, hali ambayo itaondoa malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa.

Hamad amesema Dk. Mahera amekishauri Kikosi Kazi kuendelea kujifunza kwa maeneo mengine kuhusu mchakato wa uchaguzi na kwamba hakuna sababu ya kujifungia ndani na kuaminishwa kuwa Tanzania kuna tatizo.

Aidha, amesema NEC imeelezea changamoto ya mawakala katika chaguzi kuwa ni jambo ambalo linahitaji kupatiwa ufumbuzi ambao utaondoa adha hiyo.

“NEC wamesema vyama vingi vinavyoshiriki uchaguzi havina uwezo wa kuweka mawakala ambapo wakashauri kuangalia namna ya kutatua changamoto hiyo, huku wakisisitiza pande zote kuheshimu sheria, taratibu, kanuni na katiba inavyoelekeza katika mchakato wa uchaguzi,” amesema.

Comments are closed