Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, ametoa siku 14 kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kupeleka mpango wa kuboresha takwimu za matibabu, ambao pia utadhibiti udanganyifu kwa kutumia mfumo wa Teknolojia Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Amesema hayo leo jijini Dodoma wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari na kueleza kuwa kumekuwepo na vitendo vya udanganyifu kwenye, mfuko huo, hali inayochangia kuyumbisha mfuko.
“Mtuletee mpango ndani ya siku 14, kuboresha takwimu za matibabu, hatutakubali NHIF itetereke tutachukua hatua, naagiza Katibu Mkuu na timu yako kuhakikisha kunaimarishwa mfumo wa TEHAMA, ili kudhibiti ubadhilifu,” alisema.
Alisema kuwa kuanzia sasa hawatamvumilia mtoa huduma mwenye vitendo vya udanganyifu, kwani asilimia 70 ya hospitali zinapata fedha kutoka NHIF.
Alisema kuwa baadhi ya watoa huduma wamekuwa wakifanya udanganyifu na baadhi yao wameshachukuliwa hatua.
Alisema kuwa uwepo wa mfumo wa takwimu za matibabu utapunguza gharama kwa Mfuko.
“Kama mtu alifanyiwa kipimo Bombo kwa nini afanyiwe tena Muhimbili, mfumo huo ukiwemo utasaidia kuwepo kwa taarifa za mgonjwa kwenye ngazi ya Mkoa” alisema.
Pia alisema kumekuwa na udanganyifu kwa wanachama kuwatoa wategemezi na kuwaingiza watu wengine .
“Kuna mwingine anamtoa mtoto kisa haumwi halafu anamuingiza baba mkwe mgonjwa…. Maana ya Bima ya Afya wengi wanachangia kwa ajili ya wachache wanaoumwa,” alisema
Katika hatua nyingine Waziri Ummy ametoa angalizo akisema nchi inashuhudia ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza huku mfuko huo ukiwa katika hatari ya kuelemewa na mzigo wa magonjwa hayo kwa rasilimali fedha na watu ikiwemo saratani, magonjwa ya moyo, figo na mengine.
“Gharama za kuhudumia wagonjwa wanaopatiwa tiba ya kemikali dawa na mionzi kwa mwaka 2015/16 ni shilingi bilioni 9 na mwaka 2021/22 tunalipia shilingi bilioni 22.5 hili haliendani na ongezeko la wanachama wa NHIF,” amesema.
Amesema huduma za matibabu ya figo tumetoka zilitumia shilingi bilioni 9.5 lakini kwa mwaka 2021/22 zimetumika shilingi bilioni 35.42 ambapo ilitoka idadi ya wagonjwa 280 na sasa wamefikia wagonjwa 2099.