Tamaduni zinatofautiana na kinachoashiria urembo kwa mwanamke
Suala la urembo wa mwanamke limekuwepo kwa miaka na mikaka jamii tofauti duniani zikiwa na vigezo tofauti vya urembo wa mwanamke.
Jamii zikitofautiana na kipi kinachoonyesha urembo wa mwanamke, mfano kile waafrika wanaona ni urembo kwa mwanamke wazungu huona ni kujiharibu maumbile.
Kutoka zama, wanawake wamekuwa wakitumia vitu tofauti kuongeza muonekano wao iwe ni kwa kuvaa vipuli, bangili, shanga, au hata Vidani.
Kuna jamii tofauti duniani ambazo bado zimeshikilia tamaduni zao, na wanawake katika jamii hizo bado hujipodoa na kuvaa vito vya kitamaduni, mfano jamii za wamasaai, Turkana na Mijikenda nchini Kenya, jamii ya Mursi nchini Ethiopia na jamii ya Himba nchini Namibia.
Katika karne hii, wanawake wengi hawatumii vipodozi walivyotumia wavyere, wao hutumia lipstick, kubandika kope, kuvaa mawigi na hata kubandika kucha.
Vigezo vya urembo vimebadilika kutoka zama za mababu zetu na vigezo vya urembo kwa wakati huu. Na kila jamii nayo ina vigezo vyake, unachoona kuwa urembo kwa mwanamke mwingine anaona hajatosha!