Kiongozi wa ODM nchini Kenya Raila Odinga amerejea nchini humo kufuatia kukamilika kwa ziara yake ya wiki moja nchini Uingereza.
Raila aliwasili jana Jumanne pamoja na washirika wake wa Azimio la Umoja ambao ni; Magavana Hassan Joho (Mombasa), Charity Ngilu (Kitui), Seneta James Orengo, Mbunge Junet Mohammed na aliyekuwa Mbunge wa Gatanga Peter Kenneth pamoja na mkuu wa COTU Francis Atwoli, waliokuwa wameandamana naye.
Wakati wa ziara yake nchini Uingereza, Odinga alikutana na Askofu Mkuu wa Canterbury Justin Welby na kutoa hotuba katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola na Taasisi ya Kifalme ya Masuala ya Kimataifa, Chatham House.
Ziara hiyo ambayo imekamilika inakuja miezi mitano tu kabla ya uchaguzi wa Agosti ambapo anaongoza Azimio-One Kenya kama kinara.
Huku humu nchini, kikosi chake cha waaminifu cha Azimio kinachoongozwa na katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna, Seneta wa Narok Ledama Ole Kina na Mbunge wa Kieni Kanini Kega wamekuwa wakizunguka nchi nzima huku wakipigia debe kumuunga mkono Odinga.
Odinga sasa anatarajiwa kurejesha kampeni za Azimio kwa msururu wa mikutano ya hadhara kuanzia Ijumaa, Machi 25 katika eneo la Bonde la Ufa ambalo linachukuliwa kuwa ngome ya kisiasa ya mpinzani wake mkuu Naibu Rais William Ruto.
Waziri mkuu huyo wa zamani atarejea katika eneo la Magharibi mwa Kenya ili kuwavutia wapiga kura kabla ya uchaguzi ujao.
Waziri Mkuu huyo wa zamani alianza safari ya ng’ambo Machi 14 ambapo alifanya mikutano kadhaa huku akieleza mpango wake na maono yake kwa nchi iwapo atachaguliwa kuwa rais wa 5 kuja Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.