Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) imetoa bei mpya za nauli kwa watu wazima wanaosafiri katika njia kuu na mlishi zilizoanza kutumika leo ambazo zimeidhinishwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Meneja Uhusiano wa Dart, William Gatambi, viwango vya bei zilizotolewa kwa watu wazima vinaonesha kwa njia kuu kutoka Kimara kwenda kivukoni, Morocco na Gerezani ni Sh 750 na wanafunzi 200 na kutoka Ubungo kwenda Kivukoni na Gerezani 750 na kutoka Morocco kwenda Kivukoni na Gerezani 750 na kwa wanafunzi ni Sh 200.
Wakati hapo awali viwango vya nauli kwa njia ya kuu kutoka Kimara kwenda Kivukoni, Morocco na Gerezani ilikuwa Sh 650 kwa watu wazima na kwa wanafunzi ilikuwa Sh 200 na kutoka Ubungo kwenda Kivukoni na Gerezani ilikuwa 650, wanafunzi ilikuwa Sh 200.
Na kwa njia ya mlishi kutoka Kimara kwenda Mbezi Sh 500, kutoka Kimara kwenda Kibaha na Mloganzila 700 na kutoka Gerezani kwenda Muhimbili 750 na upande wa wanafunzi 200.
Awali kwa njia mlishi ilikuwa kutoka Kimara kwenda Mbezi Sh 400, kutoka kutoka Gerezani kwenda Muhimbili Sh 650 na kwa wanafunzi Sh 200.
Dart imesema mabadiliko ya nauli hizo ni kwa mujibu wa sheria ya LATRA, ambayo ina jukumu la kupanga nauli za vyombo vinavyotoa huduma za usafiri ardhini.