Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Papa Francis aeleza aibu iliyolikumba kanisa Katoliki kuhusu unyanyasaji wa kingono. - Mwanzo TV

Papa Francis aeleza aibu iliyolikumba kanisa Katoliki kuhusu unyanyasaji wa kingono.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ameelezea aibu iliyolikumba kanisa hilo pamoja na yeye mwenyewe kutokana na kiwango cha unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto uliofanywa na kanisa nchini Ufaransa. 

Matamshi hayo ameyatoa leo mjini Vatican katika mahubiri yake ya kila Jumatano kwa waumini ambapo amezungumzia takriban watoto 330,000 wa Ufaransa ambao walinyanyaswa na mapadri na viongozi wengine wa kanisa hilo kuanzia miaka ya 1950. 

Amesema idadi hiyo ni kubwa na kwamba anaelezea masikitiko yake na mateso ya kiwewe ambayo wahanga hao wamekuwa nayo. 

Papa Francis amewataka maaskofu wote na viongozi wa kidini kuchukua hatua zote muhimu ili kuzuia vitendo kama hivyo visijirudie tena. 

Aidha, papa pia amewataka Wakatoliki wa Ufaransa kuhakikisha kwamba kanisa linabaki kuwa nyumba salama kwa wote.

Hivi karibuni ripoti ya uchunguzi juu ya unyanyasaji wa kingono nchini Ufaransa imefichua kuwa watoto wapatao 330,000 wamekuwa wakinyanyaswa kingono katika kanisa katoliki la Ufaransa kwa zaidi ya miaka 70 iliyopita.

Mkuu wa tume iliyotoa ripoti hiyo Jean-Marc Sauve amesema idadi hiyo ya watoto walionyanyaswa kingono, kulingana na utafiti wa kisayansi, inahusisha unyanyasaji uliofanywa na mapadri, makasisi pamoja na wafanyikazi wa kawaida katika kanisa hilo. 

Ufichuzi huo ni wa hivi karibuni kulitikisa Kanisa Katoliki baada ya kuzongwa na kashfa za unyanyasaji wa kingono duniani, mara nyingi zikihusisha watoto, kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita.