Jiji la Paris linatazamiwa kumuenzi mwanariadha wa Olimpiki wa Uganda aliyeuawa, Rebecca Cheptegei kwa kulipa jina lake uwanja wa michezo, meya wa mji mkuu wa Ufaransa Anne Hidalgo alitangaza Ijumaa.
Cheptegei, ambaye alishiriki katika mbio za marathon za wanawake wakati wa Michezo ya Olimpiki ya Paris mwezi uliopita, alifariki dunia kutokana na majeraha makali ya moto, siku ya Alhamisi, baada ya kumwagiwa petroli na kuchomwa moto na mpenzi wake nyumbani kwake nchini Kenya.
“Alitushangaza hapa Paris. Tulimwona. Uzuri wake, nguvu zake, uhuru wake, na ilikuwa ni kwa namna yoyote ile uzuri wake, nguvu na uhuru ambao hauruhusiwi kwa mtu aliyefanya mauaji haya,” Hidalgo aliwaambia waandishi wa habari.
“Paris haitamsahau. Tutaweka wakfu ukumbi wa michezo kwake ili kumbukumbu yake na hadithi yake ibaki miongoni mwetu na kusaidia kubeba ujumbe wa usawa, ambao ni ujumbe unaobebwa na Michezo ya Olimpiki na michezo ya Walemavu,” Hidalgo aliongeza.
Cheptegei, 33, alicheza kwa mara ya kwanza katika Olimpiki katika mbio za marathon za wanawake kwenye Michezo ya Paris, ambapo alimaliza wa 44.
Polisi na madaktari wanasema aliachwa na asilimia 80 ya majeraha ya moto baada ya kushambuliwa mbele ya watoto wake siku ya Jumapili na mwanamme raia wa Kenya, Dickson Ndiema Marangach, aliyetajwa kuwa mpenzi wake.