Pasi za kusafiria kikwazo kwa Wakenya wanaopiga kura uchaguzi wa Kenya

Takribani Raia milioni 22 wa Kenya leo wanatarajiwa kupiga kura kuchagua viongozi wa Serikali Kuu na serikali za mitaa. Kwa Wananchi wa Kenya  watapiga kura sita ambapo watamchagua Rais, Gavana wa Kaunti, Seneta, Mbunge, Mwakilishi wa wanawake bungeni na Diwani

Zoezi hilo pia linaendelea nchini Tanzania kwa Wakenya wanaoishi nchini humo, lakini changamoto kubwa iliyojitokea wakati zoezi hilo likiendelea ni kukosekana kwa pasi za kusafiria za zamani kwa baadhi ya raia wa taifa hilo wanaoishi Tanzania, kumekuwa kikwazo kwao kutekeleza haki hiyo ya kikatiba.

Upigaji kura huo umefanyika leo Agosti 9, 2022 katika Ubalozi wa Kenya nchini Tanzania, ukihusisha vituo viwili vilivyoandikisha wapigakura 496 kila kimoja kwa Jiji la Dar es Salaam.

Akizungumzia changamoto katika upigaji kura huo, Said Suleiman anayeishi Kibaha, amesema maofisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) wamemzuia kutekeleza hilo kwa kutokuwa na pasi ya zamani.

“Nimezuiliwa kupiga kura kwa sababu pasi niliyoitumia sio ile niliyokuwa nimesajiliwa zamani, lakini tangu juzi wakati tunaelimishana kuhusu kupiga kura walisema pasi mpya inaruhusiwa.

“Kwa sababu namba za pasi ya kusafiria ya zamani zinaendana na pasi mpya, lakini leo wanatwambia haiwezekani na nimemfuata ofisa mmoja anasema hawakujua kama haiwezi kutumika,” amesema.

“Sijapenda kabisa, naenda nyumbani sijapiga kura sina amani kabisa wanataka “passport” ya zamani wakati yenyewe imeexpire”

“IEBC haijabadilika yaani iko palepale zero plus zero inakuja zero yaani”-Shadrak Nzuki

Alipoulizwa kuhusu hilo, Msimamizi wa upigaji kura wa Kituo hicho, Samwel Omwangi amesema kabla ya upigaji kura raia hao wanaoishi Tanzania walipewa muda wa kusajili pasi mpya.

Amesema tangu kuanzia Septemba mwaka jana hadi Machi mwaka huu, raia hao walipewa nafasi ya kusajili pasi hizo ili zitumike, lakini baadhi yao hawakutekeleza hilo.

Pamoja na hayo kumeshuhudiwa Wakenya wengi wakifika katika eneo hilo kwa ajili ya kushiriki zoezi hilo, huku hali ya ulinzi na usalama ikiwa shwari.

Kwa mujibu wa Samweli ni kwamba kituo hicho kilifunguliwa majira ya saa 12 asubuhi na zoezi la upigaji kura litasitishwa saa 11 jioni

Uchaguzi Mkuu nchini Kenya hufanyika kila baada ya miaka mitano. Katika miaka ya hivi karibuni Kenya  imekuwa ikikumbwa na mizozo wakati wa uchaguzi, kwa mfano shuhudio la uchaguzi wa urais mnamo mwaka 2007.

Wanaowania urais nchini Kenya ni Raila Odinga wa  Azimio La Umoja, William Ruto wa Kenya Kwanza, George Wajackoyah wa Chama cha Roots na David Waihiga wa Chama cha Agano.