Balozi Humphrey Polepole, aliyewahi kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ameibuka kwa mara nyingine tena hadharani na kuikosoa vikali hali ya kisiasa ndani ya chama hicho, akisema kuwa kimeanza kupoteza mwelekeo na kusimamiwa na watu wasiokuwa na maadili ya chama.
Katika ujumbe alioutoa kwa njia ya video kupitia ukurasa wake wa Instagram, Polepole ameeleza kwamba baadhi ya watu ndani ya chama, aliowaita “wahuni”, wamekuwa wakihamishia shughuli za chama nje ya utaratibu rasmi, hali ambayo amesema ni hatari kwa ustawi wa taifa.
“Mimi mwenzenu nimefikia uamuzi wa kusema nijitoe Muhanga kusimama miongoni mwenu na kusema kuna mambo hayako sawa, yako vibaya, tuyarekebishe kwa ustawi wa chama chetu… Wajanja wachache mimi nawaita wahuni, wanapokuwa wanakipiga copy na shughuli zote zinafanyika nje ya chama… kinakuwa laana kwa nchi yetu,” alisema Polepole.
Kiongozi huyo wa zamani wa CCM alisema kwamba hali ya sasa si mtazamo wake binafsi tu, bali hata wanachama wa kawaida wa chama hicho hawaungi mkono kile alichokiita “kudhoofishwa kwa makusudi” kwa chama kwa faida ya watu wachache.
“Mimi najua wanachama wa kawaida wa CCM hawakubaliani chama chetu kinapodhoofishwa makusudi kwa maslahi ya watu wachache wasioipenda nchi yetu na wanaotenda kwa maslahi yao binafsi,” aliongeza.
Katika kauli yake, Polepole alimwelekezea lawama Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan, akisema ana mamlaka ya kufanya mabadiliko ya haraka ndani ya chama na kwamba hatua hiyo haipaswi kuchukua muda mrefu.
“Mimi niendelee kutoa rai, kwa viongozi wetu kuanzia Mwenyekiti wa CCM (Rais Samia Suluhu)… Mwenyekiti anayo turufu ya kuturekebishia chama chetu na ni uamuzi hautaki miaka, hautaki miezi, hautaki wiki… Nilikuwepo najua kwa hiyo siyo kitu nakibumbabumba hapana,” alisema Polepole.
Polepole alisema kuwa ni lazima chama hicho kijitathmini upya ili kiendelee kuwa taasisi imara inayoweza kusimamia serikali, akionya kuwa chama legelege hakiwezi kutekeleza wajibu huo.
“Wakati mwingine watu wanaweza wasielewe lakini huu ndio wakati wa chama chetu kujifanya kipya ili kikubalike mbele ya umma… chama legelege hakiwezi kusimamia Serikali, tunayo nafasi,” alisema.
Katika sehemu ya ujumbe wake, Polepole alionekana kuguswa na hali ya kisiasa inayowakumba baadhi ya viongozi aliowahi kuwaona kama walezi wake kisiasa, na kusema kuwa misingi aliyopewa na viongozi hao haikubaliani na mwenendo wa sasa.
“Nimesikia baadhi ya watu wakubwa, ninaowapenda ninaowaheshimu… mambo mema yanakuwa na kiwango cha juu wakati wote, hauwezi kupanda mambo mengine sasa hivi kwangu,” alisema kwa hisia.
Akiwaelekeza viongozi wa chama chake, Polepole alikataa vikali wazo la kurudia kauli ya “Mama apewe kumi,” akisisitiza kuwa mwaka huu si wa mtu binafsi, bali ni wa taasisi ya CCM.
“Mambo yanavyokwenda hayakubaliki tubadilishe, turekebishe pale kwenye chama… mwaka huu sio kuhusu kusema unajua Mama Samia nae apewe kumi, noooo sio kuhusu Mama Samia ni kuhusu Chama cha Mapinduzi… chama kwanza mtu baadae,” alisema kwa msisitizo.
Katika kilele cha ujumbe wake, Polepole alihoji ni kwa vigezo gani chama kitampeleka Rais Samia mbele ya wananchi kama mgombea, akisema haijulikani ni ahadi zipi mpya atakazozitoa ilhali alishakuwa Makamu wa Rais na sasa Rais.
“Tunapoenda kwenye uchaguzi saa hizi tunakwenda na Mama Samia… tunaenda kuwaambia nini kwamba ni kitu gani ambacho alitakiwa kukifanya akiwa Makamu wa Rais, ni kitu gani ambacho alitakiwa kukifanya akiwa Rais hakukifanya atakifanya miaka mitano inayokuja… haya maneno ni magumu lakini nataka tuambiane ukweli,” alisema Polepole.
Kauli za Polepole zimeibua mjadala mpana mtandaoni, ambapo baadhi ya wachambuzi wa siasa wanatafsiri matamshi hayo kama dalili ya mgawanyiko wa ndani kwa ndani unaoendelea kukikumba chama tawala kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.