
Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, ameibua mjadala baada ya kuitwa na Jeshi la Polisi kupitia Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), ili kutoa maelezo na ushahidi kuhusiana na tuhuma alizozitoa mitandaoni.
Katika kauli yake ya majibu kwa wito huo, Polepole amesema anauchukulia kwa sura mbili; upande wa kwanza akiwaona Polisi wana dhamira njema ya kusikiliza na kukusanya ushahidi, lakini upande wa pili akihisi kuna mbinu na nia ovu zinazoweza kuhatarisha usalama wake.
Akizungumza kwa njia ya mtandao Septemba 18, 2025, Polepole alisema amepokea taarifa za kuitwa kwake na anashukuru kwamba Jeshi la Polisi limeonyesha kusikiliza kilio cha wananchi kwa kuona viashiria vya makosa ya jinai kwenye yale aliyoyabainisha hadharani.
“Hili ni jambo jema na huu ni upande mmoja. Kwa sababu ukisikia Jeshi la Polisi limeona kuna viashiria vya jinai na linataka uongezee ushahidi, hiyo ni hatua ya kuonyesha kuna nia njema na dhati,” alisema Polepole.
Hata hivyo, aliongeza kwamba kuna upande wa pili wenye nia ovu, akieleza kuwa baadhi ya watu wanataka afike Polisi ili akamatwe au apotee.
“Kuna watu wanataka niende pale Polisi. Ukifika pale unakamatwa, kwa sababu hakuna sehemu wamesema kuna tuhuma kwangu. Unaweza ukaachiwa halafu baadaye unapotea na Polisi hawahusiki,” alisisitiza.
Polepole pia alihoji kwa nini wito huo usitekelezwe kwa njia ya kisasa, mfano kupitia mawasiliano ya mtandaoni, badala ya kumtaka afike moja kwa moja ofisi za Polisi. “Kwa nini wasinihoji kwa njia ya mtandao? Kama kweli nia ni kupata maelezo, teknolojia ipo. Lakini wakisisitiza lazima niende ofisini, inatia shaka,” alisema.
Kwa mujibu wake, wananchi wengi pia wana mashaka na wamekuwa wakimtumia ujumbe mitandaoni wakimwomba aendelee kuzungumza.
“Wananchi huko mtaani wana mashaka kweli na hii kitu inanifanya nijiulize maswali mengi. Watu ni waoga mno, wanakutumia ujumbe mtandaoni wakisema ‘samahani endelea kusema’, hii inaumiza,” aliongeza.
Aidha, Polepole alidai kuwa jeshi hilo limemtafuta mara kadhaa bila mafanikio, jambo linaloibua maswali zaidi. “Kama kuna mtu ndani ya Serikali anayenitaka, inawezekana kweli akamkosa Polepole kwa njia ya mawasiliano? Hii nayo inaleta maswali,” alisema.
-Polisi Walisemaje?-
Kwa upande wa Jeshi la Polisi, kupitia Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), wamesema wito huo umetolewa ili Polepole aweze kufika na kutoa maelezo ya kina pamoja na ushahidi kuhusu tuhuma alizoziweka hadharani kupitia mitandao ya kijamii.
Polisi wanasema hatua hiyo ni sehemu ya majukumu yao ya kuchunguza tuhuma zozote zinazohusiana na viashiria vya makosa ya jinai. Wameeleza kuwa mtu yeyote anapotoa madai mazito hadharani, anatakiwa pia kuonyesha uthibitisho ili kurahisisha uchunguzi.
Aidha, jeshi hilo limeeleza kuwa limekuwa likifanya jitihada za kumpata Polepole ili kutoa ushahidi wake, na kwamba hatua hiyo ni ya kawaida kisheria kwa mtu yeyote anayetoa taarifa zinazoweza kugusa masuala ya jinai.
Kuitwa kwa Polepole kumekuja wiki kadhaa baada ya kuibua hoja nzito mtandaoni akihusisha baadhi ya masuala ya kiutendaji serikalini na akisisitiza umuhimu wa uwazi na uwajibikaji.
Kadhalika amekuwa akikosoa utendani ndani ya chama chake cha CCM, na uongozi mzima uliopo sasa akiwemo Mwenyekiti wake ambaye ambaye ni Rais Samia Suluhu Hassan.
Hali hii imeibua mjadala mpana miongoni mwa wananchi mitandaoni, ambapo wapo wanaomuunga mkono wakisema anapaswa kulindwa na kusikilizwa, na wengine wakimtaka afuate taratibu na kuwasilisha ushahidi wake rasmi kwa vyombo vya dola.