Jeshi la Polisi limeanza uchunguzi wa tukio la mwili mtoto, Telesphore Mwakalinga (4) aliyeokotwa usiku wa kuamkia leo Alhamisi, Julai 18, 2024 eneo la nyumba 300, Kisasa jijini Dodoma akiwa hana mkono na sehemu za siri.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Theopista Mallya amesema tukio hilo lilitokea jana Jumatano usiku kwenye nyumba 300 zilizopo Kisasa jijini Dodoma.
“Jana askari polisi akiwa katika eneo hilo aliona mbwa akiwa na kitu, jambo ambalo lilimfanya kusogelea karibu na kumuona mtoto huyo. Alitoa taarifa polisi ambao walikwenda kwenye tukio na kumpeleka hospitali,” amesema.
Kamanda Mallya amesema sasa hivi hawawezi kusema mtoto huyo aliuawa ama vinginevyo hadi hapo watakapopata uhalisia wa tukio hilo baada ya uchunguzi kukamilika.
“Siwezi kusema ameuawa hadi tutakapokamilisha uchunguzi wa tukio hilo yakiwemo mazingira ya tukio lenyewe ikiwa aliondokaje nyumbani,” amesema kamanda huyo.
Vyanzo mbalimbali vya habari vimeeleza kuwa, mtoto huyo alipotea jana jioni saa 12.00 jioni lakini alipatikana saa 4.00 usiku, akiwa hana mkono mmoja na sehemu za siri katika eneo hilo la nyumba 300 za Kisasa jijini Dodoma.
Kamanda Theopista amesema mwili wa mtoto huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.