Polisi jijini Mwanza yakamata kilo 561 za mirungi

Jeshi la Polisi mkoani Mwanza nchini Tanzania limekamata gari aina ya Toyota Harrier ikiwa limebeba kilo 561 za mirungi.

Akizungumza na waaandishi wa habari leo Kamanda wa Polisi mkoani humo, Ramadhani Ng’anzi amesema gari hilo mali ya Malema Maswi lilikamatwa Juni 8, 2022 Saa 5: 20 usiku katika maeneo ya Itumbili wilayani Magu mkoani humo muda mfupi baada ya kutelekezwa na dereva ambaye jina lake halijatambulika.

“Gari hilo iliyokuwa inatokea mkoani Mara ilipofika kwenye kizuizi cha magari wilayani Magu askari walilitilia shaka wakalisimamisha lakini dereva alikaidi amri na kupita kizuzi jambo lililosababisha tairi zake kupasuka. Lilipofika umbali wa mita 600 dereva alisimamisha na kukimbia lakini upekuzi ulipofanyika tukakuta kuna mirungi,” amesema Ng’anzi

Amesema jeshi hilo linamshikilia mmiliki wa gari kwa mahojiano kuhusiana na tuhuma za usafirishaji wa dawa hizo huku akisema msako wa kumkamata dereva unaendelea.

“Hiki ni kiwango kikubwa cha dawa za kulevya ambacho tunaamini kama kingeingia hapa jijini kingeleta madhara kwa wananchi. Sheria ya dawa ya kulevya iko wazi kwamba chombo chochote kitakachotumika kwenye usafirishaji kinaweza kutaifishwa,” amesema Ng’anzi

Kamanda Ng’anzi amesema kundi lililoathirika kwa kiasi kikubwa na matumizi ya dawa hizo mkoani humo ni vijana huku akisema jeshi hilo linaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na madhara ya matumizi ya dawa hizo.

“Tumebaini kwamba wanawake nao wameanza kujiingiza kwenye matumizi ya dawa hizi kidogo kidogo kundi ambalo awali tuliamini ni watu waaminifu hii inaashiria kuna mmonyoko wa maadili kwenye suala hili tutasimamia sheria bila kuangalia hali wala jinsia ya mtu,” amesema Ng’anzi