Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha nchini Tanzania kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi, vimeanza uchunguzi kuhusu kifo cha fundi magari, Kibabu Msese (26), mkazi wa Karatu, ambaye alikuwa miongoni mwa watuhumiwa wa unyang’anyi wa kutumia silaha.
Kutokana na hali hiyo, polisi imewataka ndugu wa marehemu kuwa watulivu wakati Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vikiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo ameyasema hayo leo Juni 2, 2022 kuwa taarifa za awali zinaonesha marehemu alikamatwa na watu wengine wanne kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha lililotokea Mei 11, 2022 usiku, eneo la Manyara Kibaoni, Karatu.
Amesema siku hiyo Innocent Olotu, mfanyabiashara wa huduma za kifedha za simu alivamiwa na kundi la majambazi na kuporwa kiasi cha shilingi 14,590,000, simu kadhaa, pamoja na mashine za uwakala wa benki.
“Ufuatiliaji ulifanyika na kuwakamata watuhumiwa mbalimbali ndani na nje ya mkoa wa Arusha, wakati wa mahojiano watuhumiwa hao walionesha baadhi ya mali zillizoibwa pamoja na silaha waliyokuwa wanaitumia katika tukio hilo, ambapo pia walikiri kushiriki matukio kadhaa nje na ndani ya Mkoa,” amesema.
Ameeleza kuwa watuhumiwa walifikishwa mahakamani Mei 27 mwaka huu na kwamba watuhumiwa wengine wanaendelea kutafutwa.
Amesema marehemu alikuwa ni mmoja wa watuhumiwa hao, hali yake ilibadilika na kukimbizwa hospitali ya Karatu Mei 24, kisha Mei 25 alipelekwa hosptali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha kwa matibabu zaidi, ambapo mauti yalimkuta Mei 31, akiendelea na matibabu.
“Uchunguzi umeanza kwa kushirikisha vyombo vingine kubaini chanzo cha kifo hicho, mwili wa marehemu umehifadhiwa hosptali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru,” amesema Kamanda.