Jeshi la Polisi Tanzania limesema halijapiga marufuku kufanyika mikutano ya hadhara na ile mikutano ya ndani ili mradi inafuata sheria za nchi.
Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa leo na Jeshi la Polisi Makao Makuu ni kwamba kilichopigwa marufuku ni mkusanyiko uliokuwa umeitishwa na viongozi wa CHADEMA jijini Mbeya kwa kivuli cha kuadhimisha siku ya Vijana Duniani.
Kanusho hilo kutoka Makao Makuu ya Polisi limekuja kufuatia taarifa ya Polisi Mbagala iliyoandikwa kwenda kwa chama cha ACT Wazalendo kuzuia mkutano wa hadhara wa vijana wa chama hicho waliopanga kufanya leo Agosti 12,2024.
Katika sehemu ya taarifa ya taarifa hiyo ya Polisi Mbagala kwenda kwa ACT Wazalendo ilinukuliwa ikieleza”Napenda kukujulisha kuwa mikutano yote ya hadhara na ya ndani imezuiliwa hadi hapo yatakapotolewa maagizo maelekezo mengine”
Tamko hilo liliibua hisia mseto na mijadala mitandaoni ikiwa katikati ya tukio la kamatakamata la viongozi wa CHADEMA.
Hata hivyo saa kadhaa kupita wakati mjadala huo ukiendelea Polisi Makao Makuu wakakanusha tamko la Polisi Mbagala.