Polisi Tanzania: Wengi wanaoripotiwa kutekwa hujificha kwa sababu binafsi

Jeshi la Polisi Tanzania limeeleza kuwa sehemu kubwa ya matukio ya watu kuripotiwa kupotea au kutekwa nchini humo hayahusiani na vitendo halisi vya utekaji, bali yamesababishwa na sababu za kibinafsi kama mapenzi, migogoro ya kifamilia, imani za kishirikina na ukwepaji wa madeni.

Katika taarifa iliyotolewa leo Jumatano tarehe 18 Juni 2025, ambayo imeeleza baadhi ya matukio hayo,  polisi wamesema uchunguzi wa kina umebaini kuwa watu wengi waliodaiwa kutekwa ama walikuwa wamejificha kwa hiari, walitoroka kutokana na sababu mbalimbali au walihusika katika vitendo vya uhalifu kabla ya kupotea kwao.

“Huwezi kusema moja kwa moja mtu aliyeripotiwa kupotea ametekwa au kuuawa bila ushahidi wa kuthibitisha,” ilisema taarifa hiyo ya Jeshi la Polisi, ikisisitiza kuwa wanachukua kwa uzito kila taarifa ya kupotea kwa mtu lakini lazima uchunguzi wa kina ufanyike.

Tukio lililovuta hisia – Shekhe aliyedai kutekwa

Miongoni mwa matukio yaliyopewa uzito ni tukio la tarehe 2 Juni 2025, ambapo Shekhe Zuberi Said Nkokoo (53), mwalimu na kiongozi wa taasisi ya dini, aliripotiwa kutekwa usiku akiwa na fedha taslimu kiasi cha shilingi milioni 42.

Baadaye, uchunguzi wa polisi ulionyesha kuwa hakutekwa bali alitoweka kwa hila ili kukwepa kulipa deni la zaidi ya shilingi milioni 521 alilodaiwa na watu mbalimbali. Jeshi la Polisi limesema Shekhe huyo atafikishwa mahakamani baada ya taratibu kukamilika.

Katika tukio jingine, Ritha Severine Ndambailo kutoka Mtwara, aliripotiwa kutekwa lakini uchunguzi ulionesha kuwa aliuawa kutokana na wivu wa mapenzi. Watuhumiwa wawili wamekamatwa.

Ezania Kamana (36) aliyepotea Agosti 2024, alikutwa ameuawa na mpenzi wake. Mwili wake ulikatwa vipande na kutupwa kwenye mifuko ya plastiki katika maeneo ya Ununio, Dar es Salaam. Mtuhumiwa alikamatwa na kesi inaendelea mahakamani.

Katika mkoa wa Singida, watu saba waliodaiwa kupotea walikutwa wameuawa kwa kukatwa viungo vyao katika kile polisi wanasema ni imani za kishirikina. Watuhumiwa kadhaa akiwemo mganga wa kienyeji walikamatwa.

Polisi pia wametoa mfano wa mtu mmoja aliyedai kutekwa ili kuficha matumizi ya mahari ya mtoto wake. Wengine walihusishwa na migogoro ya kifamilia, migogoro ya ardhi au tuhuma za wizi.

Polisi: Matukio haya yanatumika kisiasa mitandaoni

Jeshi la Polisi limeonya dhidi ya upotoshaji unaoenezwa mitandaoni, likisema kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakitumia matukio haya kwa malengo ya kisiasa au kuchochea hofu isiyo na msingi.

“Baadhi ya taarifa zinazotolewa kwenye mitandao ya kijamii zinawadanganya wananchi na kuhatarisha amani,” ilisema taarifa hiyo, ikitoa wito kwa wananchi kuwa na subira wakati uchunguzi unaendelea.

Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, mtu anayetoweka huzingatiwa kuwa amekufa baada ya miaka mitano kupita bila kupatikana, iwapo kutakuwa na ushahidi wa kuaminika.

Wakosoaji wanahoji: Je, vipi kuhusu watu maarufu waliopotea?

Ingawa taarifa ya Polisi imefafanua matukio kadhaa ya watu wa kawaida, haikugusia matukio ya awali yaliyohusisha watu maarufu kama Mdude Nyagali, mwanaharakati aliyepotea zaidi ya mwezi mmoja sasa na Mwanaharakati na mwanachama wa Chadema Deusdedith Soka aliyedaiwa kutekwa tangu Agosti 18,2024.

Mashirika ya haki za binadamu yamekuwa yakitaka uchunguzi huru kuhusu baadhi ya matukio ya watu kupotea ambayo yamekuwa yakihusishwa na mamlaka.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi limeendelea kusisitiza kuwa halihusiki na vitendo vya utekaji au uvunjaji wa haki, na kuwa hatua dhidi ya wahusika wa uhalifu huchukuliwa kwa mujibu wa sheria na ushahidi.