Search
Close this search box.
Africa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, James Manyama

Askari polisi mwenye namba F.5123 D/ CPL Subira ambaye aliyekuwa na bunduki aina ya AK 47 adaiwa kumuua Juma Ramadhani kwa kumpiga risasi na kuwajeruhi watatu wakati akiwa kwenye harakati za kujihami kwenye vurugu zilizotokea katika kiwanja cha mpira cha Lake Tanganyika mkoani Kigoma, nchini Tanzania.

Vurugu hizo zilitokea jana Jumatatu Machi 14, 2022 majira ya saa 10 jioni wakati wa fainali ya mchezo wa mpira wa miguu wa kumuenzi Dk Living Stone baina ya timu ya Mwandiga Fc dhidi ya Kipampa Fc ya Ujiji ulioandaliwa na Shirika la Joy in The Harvest kwa kushirikiana na Chama cha Mpira wa Miguu Kigoma (KFA) na mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Ester Mahawe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, James Manyama amesema marehemu Juma amefariki dunia akiwa hospitalini akiendelea na matibabu.

Kamanda Manyama ameyasema hayo leo Machi 15,2022, wakati akizungumza na wanahabari na kwamba vurugu hizo zilitokea kipindi cha kwanza wakati Mwandiga Fc iliyokuwa ikiongoza kwa goli moja liliposawazishwa na Kipampa Fc ambapo mashabiki wa Kipampa Fc  kuvamia jukwaa la mashabiki wa timu ya Mwandiga na kuanza kuwazomea huku wakiwarushia chupa za maji na mawe hali iliyosababisha kuibuka kwa vurugu.

Amesema baada ya vurugu hizo kutokea askari waliokuwa wamepangwa kwa ajili ya kuimarisha ulinzi walijitahidi kudhibiti vurugu hizo lakini walizidiwa nguvu na kuomba msaada.

“Askari waliongezeka uwanjani pale kwa ajili ya kutuliza fujo na kutumia mabomu ya machozi na kishindo kuthibiti vurugu hizo lakini mashabiki hao waliendelea kufanya fujo” Amesema Kamanda Manyama

“Amesema mashabiki hao waliendelea kushambuliana na kuwapiga mawe askari waliokuwepo uwanjani hapo na kusababisha askari namba F.5123 D/ CPL Subira aliyekuwa na silaha aina ya AK 47 kushambuliwa sehemu ya kichwani na kuanguka chini” ameongeza kamanda Manyama

Amesema askari huyo aliamua kujihami dhidi ya tishio la kunyang’anywa silaha pamoja na kutetea uhai wake kwa kufyatua risasi tisa hewani  sambamba na kutoa  onyo la kuwatawanya mashabiki waliokuwa wakimshambulia kwa mawe.

Amesema licha ya kupiga risasi hizo lakini mashabiki hao waliendelea kumshambulia kwa mawe akiwa ameanguka chini ndipo alipofyatua risasi tatu na moja ilimpata marehemu Juma ambaye alijeruhiwa katika paja la mguu wa kushoto na risasi ya pili ilimjeruhi Omary Amdan (35), katika unyayo wa mguu wake wa kushoto na risasi ya tatu ilimjeruhi Nasibu Moshi (35), katika mguu wake wa kushoto.

Amesema majeruhi wote walikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa Maweni kwa matibabu na vurugu zilipotulia mchezo huo wa fainali uliendelea hadi mwisho.

Amesema saa 12 jioni Juma Ramadhani akiwa anapatiwa matibabu alifariki dunia huku majeruhi wawili walipatiwa matibabu na kuruhusiwa kwenda nyumbani huku askari Subiri alibakia kwa ajili ya matibabu zaidi.

Amesema kutokana na tukio hilo jeshi la polisi linawashikilia watu wanne wanaotuhumiwa kuwa chanzo cha vurugu hizo na upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea na watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria zaidi.

” Niwasihi wananchi wa mkoa wa Kigoma wakati wa ushabiki wa michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu washabikie kwa ustaarabu, kuvumiliana na kufuata sheria za nchi na kuacha kushabikia kwa mihemko inayosababisha vurugu,”amesema Kamanda Manyama.

Comments are closed