Jeshi la Polisi nchini Tanzania limedaiwa kutumia nguvu kwenye ukamatwaji wa viongozi wa Chadema na wafuasi wake kati ya Agosti 11 na 12,2024 wakati wakielekea kwenye maadhimisho ya siku ya Vijana Duniani yaliyopangwa kufanyika jijini Mbeya hapo jana chini ya Mwavuli wa Baraza la Vijana wa Chadema.
Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu Bara kutoka chama cha Chadema bwana Benson Kigaila ni kwamba katika kundi kubwa la watu takribani 500 waliokamatwa na Polisi kati ya siku hizo mbili, wakiwemo viongozi wakuu wa chama hicho ni kwamba Makamu Mwenyekiti Bara, Tundu Lissu, Katibu Mkuu John Mnyika na Mwenyekiti Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu wameumizwa vibaya kutokana na nguvu iliyotumika kuwakamata.
“Imethibitika kwamba Katibu Mkuu (John Mnyika) na Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi walipigwa sana wakati wa kukamatwa.Kilichotokea walianza kumkamata Makamu Mwenyekiti Bara (Tundu Lissu), kwa kumburuza na kumrusha kwenye gari, Katibu Mkuu alienda kuangalia kwanini wanamburuza Makamu, Kamanda wa Polisi ambaye ni Kamanda wa Operesheni na Mafunzo, akamuita Katibu Mkuu alipoenda akamnyang’anya miwani yake akaivunja mbele ya Polisi, Polisi wakaanza kumpiga”- ameeleza Kigaila kwenye taarifa aliyoitoa leo.
Agosti 12, 2024 Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Awadh Haji alitangaza kuachiwa kwa viongozi hao na baadhi ya makada huku akionya kuwa polisi haitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayekiuka sheria na taratibu za nchi kwa kuiga mataifa mengine.
Mwenyekiti Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti Tundu Lissu, Katibu Mkuu John Mnyika, Mwenyekiti wa BAVICHA John Pambalu, Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa Joseph Mbilinyi walisafirisha kutoka Mbeya hadi Dar es salaam na kuwasili asubuhi ya leo ambapo Polisi waliwapeleka hadi katika makazi yao