Polisi wakamata Jezi feki za klabu ya Simba

Jeshi la polisi Mkoani Kilimanjaro linawashikilia watuhumiwa 11 wakiwemo wafanyabaishara wa Manispaa ya Moshi, Mkoani humo kwa kuuza na kusambaza  jezi feki za timu ya Simba.

 Akizungumza na waandishi wa habari leo Kaimu Kàmanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Yahaya Mdogo amesema wamekamata jumla ya jezi 446 zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 15.6.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa  Kilimanjaro lilipata taarifa fiche kuhusu uwepo wa wafanyabiashara wa mkoa Kilimanjaro hasa Manispaa ya Moshi wakiuza  jezi feki za Timu ya mpira wa miguu ya Simba, jezi ambazo si halisi zinazotengenezwa na kampuni ya Vunjabei,”

Kamanda Mdogo amesema katika uchunguzi wa awali kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Vunja Bei, imebainika kuwa jezi hizo ni feki  kutokana na kwamba hazina ubora na ni tofauti na zinazotengenezwa na kampuni hiyo ya Vunja bei iliyopewa zabuni ya kutengeneza na kusambaza jezi za timu ya Simba.

Kamanda Mdogo amesema wanaendelea na uchunguzi na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watuhumiwa hao.

 Aidha Kamanda Mdogo amewataka wafanyabaishara kufanya biashara kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na mamlaka zinazohusika.