Search
Close this search box.
Africa

Jeshi la Polisi nchini Tanzania limetoa ufafanuzi juu ya askari wake aliyejinyonga kwa tambala la deki akiwa mahabusu huko mkoani Mtwara juu ya kwanini hakuzikwa kijeshi kama ilivyo taratibu za mazishi ya askari.

Kutolewa kwa taarifa hiyo kumetokana na uwepo wa hoja nyingi zilizoibuliwa na watu mbalimbali, kwanza kuhusu tukio hilo lakini pia ni kwanini asakri huyo hakuzikwa kwa mujibu wa taratibu za kipolisi.

Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania SACP David Misime, amesema asakri yeyote aliyefariki katika hali ya kujitoa uhai hazikwi kijeshi kwa maana ya kwamba hakuna gwaride la mazishi litakalochezwa na risasi au mabomu ya kishindo kupigwa, kwani anahesabiwa sio shujaa

Askari yeyote aliyefariki katika hali ya kujitoa uhai, hazikwi kijeshi, kwani anahesabiwa kama hajafa kishujaa na hastaili heshima hiyo.Taratibu nyingine hufanyika kama kumpeleka katika eneo atakalozikwa kulingana na matakwa ya familia na ndivyo ilivyofanyika kwa askari huyu” amesema SACP David Misime 

Januari 22,2022 Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Grayson Mahembe, alikutwa amejinyonga hadi kufa akiwa ndani ya mahabusu kutokana na tuhuma za mauji ya kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Mussa Hamisi na kisha kuutupa mwili wake vichakani huko katika kijiji cha Namgogori mkoani Mtwara manamo Januari 5, 2022.

Grayson alikuwa miongoni mwa Maofisa wengine wa Polisi saba wanaotuhumiwa kuumua kijana huyo mwenye umri wa miaka (25), aliyeuawa baada ya kudai fedha zake shilingi Milioni 33.7 ambazo Maafisa hao wanadaiwa kuzichukua kutoka kwa kijana huyo baada ya kumfanyia upekuzi.

Wakati Polisi wakitoa taarifa hiyo, baba mzazi wa marehemu Grayson, mzee Gaitan Simon Mahembe ambaye pia ni mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania, amesema alipokea taarifa za mwanawe kuwa yuko mahabusu ya polisi kwa masuala ya uhalifu lakini hakujua ni uhalifu gani aliufanya mtoto wake.

Ilipofika January 22, mzee Gaitan alipokea taarifa nyingine kuwa mtoto wake amefariki kwa kujinyonga,  lakini kinachomshangaza na kumuuma, ni kwamba hakuna taarifa nzuri wala picha za ushahidi kwamba zinaonyesha ni kweli kwamba amejinyonga bali anaona taarifa za polisi zinagongana.

“Katika familia Gyrayson ni mtoto wangu wa tatu, mimi nina watoto wanne wakike wawili na wakiume wawili sasa nitabaki na watatu baada ya huyu marehemu kuniacha katika mazingira ya kutatanisha” amesema mzee Gaitan na kuongeza kuwa 

“Katika moja ya vifo amabavyo sitavisahau ni pamoja na hiki, kwa sababu bora ningeuguza au ningepewa taarifa kuna hiki na hiki.Lakini mpaka tarehe 21 ni mzima tarehe 22 napewa taarifa za kujinyonga tena kwenye mahabusu ya polisi”

Mzee Gaitan kwa sasa jicho lake ni kwa serikali na Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina juu ya kifo cha mwanawe lakini taarifa zilizopo sasa kuhusu mwanawe hazijamridhisha kutokana na uhalisia wa tukio lenyewe.

Comments are closed