Rais Samia Suluhu Hassani amemuelekeza Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa kuunda kamati Huru itakayofanya uchunguzi wa mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi mkoani Mtwara
Rais Samia ameyasema hayo leo akiwa Magu mkoani Mwanza wakati akielekea mkoani Mara kwa ziara ya kikazi ya siku nne, ambapo akiwa njiani rais Samia alisimama kusalimiana na wananchi na kusikiliza kero zao.
Rais Samia amesikitishwa sana na mauaji yanayendelea kutokea hapa nchini lakini mbaya zaidi ni yale mauaji yalifoanywa na jeshi la polisi mkoani Mtwara ambapo amesema jeshi hilo haliwezi kujifanyia lenyewe uchunguzi isipokua lazima kamati huru iuhusishwe.
“Mauaji yametokea Mtwara na kwa taarifa zilizopo, Jeshi ndilo lililofanya mauaji.Taarifa niliyonayo ni kwamba, Jeshi limetengeneza kamati ya kufanya uchunguzi alafu walete taarifa, haiwezekani Jeshi lifanye mauaji, Jeshi lijichunguze lenyewe.” Rais Samia
Aidha amemwambia Waziri wa Mambo ya Ndani Mhandisi Hamadi Masauni, kuwa jeshi lake linapaswa kujitafakari kuona kama hichi kilichotokea ndio misingi ya jeshi la polisi.
“Nataka jeshi lako lijitafakari waone kama kinachotokea ndio misingi ya jeshi la polisi au vinginevyo, kwa hiyo tunasubiri taarifa ya kamati huru itakayoundwa na Waziri mkuu ituletee taarifa tulinganioshe na ile ya jeshi la polisi na tuone taarifa mbili zinasemaje tuchukue muafaka” amesema Rais Samia.
Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamadi Masauni, mkoa wa Mwanza pekee kuna matukio 4 ya mauaji yaliyotokea ndani ya mwezi Januari pekee, ambapo hadi sasa jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi kuhakikisha watuhumiwa wote wa matukio hayo wanakamatwa.
Katika kipindi cha mwezi Januari 2022, matukio ya mauaji yaliyotikisa ni takribani 22, ambapo yamehusisha wivu wa mapenzi, ushirikina, tamaa ya mali na migogoro ya ardhi.