Jeshi la Polisi limetoa tahadhari kwa wananchi kuhusu kuwepo kwa kikundi cha watu kinachoandaa picha mjongeo na taarifa za matukio yaliyotokea siku za nyuma pamoja na mengine yaliyo tengwa kwa makusudi, kisha kuzipeleka kwenye mitandao ya kijamii kwa lengo la kuonyesha kwamba yametokea hivi karibuni au kwa kipindi hiki cha sasa.
Taarifa ya Jeshi la Polisi imesema kuwa baadhi ya taarifa hizo zimeandaliwa kwa uangalifu ili kuzalisha taharuki, ikiwemo kuchukua matukio yaliyotokea katika nchi nyingine, kuyatengeneza upya, kisha kuyaunganisha na sauti za Kiswahili zenye lafudhi ya nchi yetu ili yaonekane yametokea nchini.
“Pia wamepanga kuchukua picha za baadhi ya viongozi na kuyawekea maneno na sauti zenye matamko ya upotoshaji ili ionekane wao ndiyo wanazungumza au wanayatamka, hali ambayo si kweli,” imeeleza taarifa ya Polisi.
Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa wananchi wasitapeliwe na taarifa au picha hizi, na wametakiwa kupuuza vipeperushi na maandiko yanayofanana kwani yameandaliwa kwa nia ya kihalifu na lengo la kuleta taharuki, ukosefu wa amani, na kuchafua utulivu wa wananchi.
Aidha Jeshi hilo limewataka wananchi kuwa makini, kuthibitisha habari wanazopokea, na kutoeneza au kusambaza taarifa zisizo na uthibitisho, ili kuepuka kuenea kwa upotoshaji unaoweza kuathiri amani na mshikamano wa jamii.