Prof.Assad asema bora kusimamia unachokiamini kuliko kuwa na unafiki, adai maisha yake kwa sasa ni mazuri baada ya kusimamia anachokiamini

Prof. Mussa Assad, CAG wa zamani

Aliyewahi kuwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad amesema hapendi kuitwa Mstaafu na neno hilo linamchukiza, kutokana na yeye kuwa hajawahi kuwa mstaafu bali aliondolewa kazini pasipo kufatwa taratibu za kisheri.

Prof Assad ameyasema hayo leo jijini Dodoma kwenye mdahalo wa kitabu cha Rai ya Jenereli, kitabu ambacho kinazungumzia umuhimu wa Katiba Mpya nchini Tanzania.

“Sipendi sana kusikia neno mstaafu na kwamba neno hilo linaniudhi linapotamkwa mbele yangu,” amesema Profesa Assad.

Hii leo Prof Assad, anatimiza miaka 60 ya maisha yake tangu kuzaliwa kwake, na kwa mujibu wa sheria za utumishi umma pengine leo ndio siku ambayo alipaswa kustaafu utumishi wa umma.

Profesa Assad aliteuliwa na aliyekuwa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kuwa CAG Novemba 5, 2014 na aliondolewa Novemba 4, 2019 chini ya utawala wa hayati Dk John Magufuli,  kwa maelezo kuwa alimaliza muda wake.

Kabla ya kuondolewa kwake, ulizuka mvutano kati yake na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai, uliosababisha Profesa Assad kufikishwa kwenye Kamati ya Bunge ya Haki, maadili na madaraka ya Bunge akidaiwa kudharau mhimili huo kwa kauli yake kuwa Bunge ni dhaifu.

Mvutano huo ulizuaa mjadala mkubwa mitandaoni, huku wengi wao wakikosoa namna ambavyo serikali haitaki kukosolewa na kutafsiri vibaya neno dhaifu

Pengine mvutano huo ndio ulimsukuma aliyekuwa Rais wakati huo kumuondoa katika nafasi yake na kuteuliwa CAG mwingine.

Mdahalo huo umeandaliwa na kituo cha sheria na haki za binadamu (LHRC) na wasemaji ni Jenerali Ulimwengu na Profesa Mussa Assad huku makundi mbalimbali ikiwemo wabunge wameshiriki.

Prof Assad ambaye anajipambanua kama mtu anayependa kusimamia anachokiamini katika kazi yake, anasema kinachosababisha viongozi wengi kutokuwa na misimamo yao ni kutoamini wanachokisimamia na kuhofia kwamba huenda wakapoteza magari magari ya V8 waliyopewa na serikali.

Ameongeza kuwa kuondolewa kwake hakukuwa na Sababu isipokuwa kulitokana na kutosimamiwa vema kwa Katiba ya nchi licha ya kutaja namna nzuri ya kumuondoa mtu wa cheo hicho.

Anasema kwa sasa maisha yake ni mazuri baada ya kuamua kusimamia kile anachokiamini kuliko kuwa na unafiki kama baadhi ya watu wanaotaka kujipendekeza kwa sababu ya kuwa na magari V8.