Search
Close this search box.
Africa

Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linawashikilia watu 11 akiwemo raia wa China, Meng Zhaon Ming (29) kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa saruji  na mafuta aina ya Diesel katika mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Mwanza hadi Isaka mkoani Shinyanga .

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema Ming ambaye ni mtunza stoo anashikiliwa na wenzake sita kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa mifuko 390 kwenye mradi wa SGR huku mmoja akikutwa na Lita 800 za mafuta ya Diesel kutoka kwenye mradi huo.

Kamanda Mutafungwa amesema mifuko hiyo ya saruji ni kati ya mifuko 600 inayodaiwa kuibwa katika mradi huo huku akiwataja watuhumiwa wengine katia wizi huo  kuwa ni dereva wa gari lililotumika kusafirisha saruji hiyo, Juma Maiko (29), mnunuzi wa saruji, Masele Shija (35) na mbeba mizigo aliyetumika kushusha saruji hiyo, George Abel (32).

Amewataja watuhumiwa wengine wanaoshikiliwa wa wizi huo ni mkazi wa Nyambiti mkoani humo, Emmanuel Nestory (40) Michael Samwel (29) na Nicholaus Paul (25) ambao wote walishiriki kushusha shehena ya saruji hiyo wilayani Misungwi mkoani Mwanza.

“Machi 8 mwaka huu kwenye operesheni zetu mifuko 390 ya cement aina ya Twiga mali ya SGR baada ya kumhoji alisema ameuziwa na dereva wa kampuni ya Texas ambaye alikabidhiwa saruji hiyo kutoka kwenye ghala la SGR lililoko Nyanshishi kwa ajili ya kuzipeleka Bukwimba badala yake aliiba na kuiuza kwa Masele Shija,” amesema Mutafungwa.

Pia amesema mkazi wa kijiji cha Maligisu wilayani Kwimba mkoani Mwanza, Daudi Shija (23) anayeshikiliwa kwa tuhuma za kukutwa na Lita 800 za mafuta aina ya Diesel inayodhaniwa kuibwa kwenye mradi huo.

Mbali na wizi huo, polisi mkoani hapa inamshikilia mkazi wa Nyamhongolo wilayani Ilemela mkoani hapa, Alex Josephat (24) na Kulwa Juma (20) kwa tuhuma za kuiba runinga (TV) mbili aina ya Sony inchi 42 na 43, jenereta, spika ya redio, king’amuzi cha Azam na Amplifaya aina ya Kenwood.

Katika tukio lingine, Polisi inamshikilia mkazi wa kijiji cha Izizima “A” kata ya Mhande wilayani Kwimba mkoani hapa, Nyerere Malekauo (62) kwa tuhuma za kupanda miche 60 ya Bhangi kwenye shamba lake la mahindi.

“Pia tulifanikiwa kukamata magunia matatu yaliyokuwa na bhangi ambapo watuhumiwa waliokuwa na magunia hayo walitoroka baada ya kuona polisi, upelelezi wa kina unaendelea ili kuwakamata,” amesema kamanda huyo.

Kamanda huyo pia amesema wanamshikilia dereva wa gari la kampuni ya Takbiir linalofanya safari zake kati ya Mwanza na Geita, Shabani Daudi (42) na wakala wake, Amini Upendo (52) kwa tuhuma za kukutwa na mifuko ya plastiki iliyozuiwa.

Comments are closed