Raia nchini Msumbiji leo wanafanya uchaguzi kwa ajili ya kumpata rais mpya na wabunge, huku chama cha Frelimo, ambacho kimekuwa madarakani kwa miaka 49, kikitarajiwa kuendelea kushika hatamu.
Uchaguzi huu unakuja katikati ya mvutano wa kisiasa katika taifa hilo la kusini mwa Afrika, ambalo linakabiliwa na viwango vya juu vya umasikini na ukosefu wa usawa, huku ghasia za kiusalama kaskazini zikizuia miradi mikubwa ya gesi.
Rais anayemaliza muda wake, Filipe Nyusi, mwenye umri wa miaka 65, ambaye anajiuzulu baada ya kukamilisha muda wa awamu mbili, alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kupiga kura wakati vituo vya kupigia kura vilipofunguliwa saa 1:00 asubuhi
“Ningependa pia kuomba kwamba hakuna kundi la raia litakaloshawishi au kutishia wengine, kwamba kila kitu kifanyike kwa amani na utulivu na tuwe na tahadhari kutoanzisha matokeo kabla ya wakati,” alisema Nyusi.
Baada ya uchaguzi wa mitaa mwaka 2023 ambao ulionekana kuwa wa udanganyifu, kulikuwa na maandamano katika miji mikubwa ambapo polisi waliua watu kadhaa.
Matokeo ya uchaguzi wa Jumanne, ambao pia utachagua mawaziri wa mikoa, yanatarajiwa kutangazwa baada ya takriban wiki mbili.
Mgombea wa Frelimo kuchukua nafasi ya Nyusi ni gavana wa mkoa asiyejulikana sana, Daniel Chapo, mwenye umri wa miaka 47, ambaye pia alitoa wito wa utulivu baada ya kupiga kura.
Kuchaguliwa kwake kutakuwa na maana ya mabadiliko ya kizazi: atakuwa rais wa kwanza wa Msumbuji aliyezaliwa baada ya uhuru kutoka Ureno mwaka 1975 na wa kwanza kutokuwa na uhusiano na vita vya ndani vya miaka 16 kati ya Frelimo na chama kikuu cha upinzani, Renamo.
Washindani wakuu wa Chapo ni kiongozi wa Renamo, Ossufo Momade, mwenye umri wa miaka 63. Mgombea mwingine ni Venancio Mondlane, mwenye umri wa miaka 50, ambaye alipoteza uchaguzi wa umeya mwaka 2023 chini ya bendera ya Renamo na kudai udanganyifu mkubwa wa uchaguzi. Mondlane, ambaye ni maarufu miongoni mwa wapiga kura vijana, aliondoka katika chama hicho mwezi Juni na kuungana na chama kidogo cha Optimistic Party for the Development of Mozambique (Podemos).
Mgombea mwingine muhimu ni Lutero Simango, mwenye umri wa miaka 64, rais wa harakati ya kisiasa ya Mozambique Democratic Movement, ambaye ni mkosoaji mkubwa wa Frelimo, akielezea viongozi wake kama “wezi waliovaa mavazi mekundu”, rangi ya chama hicho.
– Tunahitaji mabadiliko –
Ingawa wachambuzi walisema wana mashaka juu ya uwezekano wa uchaguzi huu kuleta mabadiliko makubwa katika nchi maskini, hili ndilo wengi wa wapiga kura walikuwa wakitarajia.
“Tunahitaji mabadiliko, tunahitaji mambo yafanye kazi,” alisema Leta Decastro, mwenye umri wa miaka 43, kwenye kituo cha kupigia kura.
“Nataka bunge libadilike,” alisema mhandisi wa misitu, Gisela Guambe, mwenye umri wa miaka 42. “Hakuna mjadala wa kutosha bungeni sasa. Upinzani unahitaji uwepo tofauti.”
Mnamo mwaka 2019, vyama vya upinzani vilipinga matokeo yaliyowapa Frelimo asilimia 73, wakitaja udanganyifu wa uchaguzi.
“Hakuna kitakachobadilika,” alisema Domingos Do Rosario, mwanafunzi wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Eduardo Mondlane mjini Maputo, akitaja taasisi dhaifu na mikataba ya kisiasa isiyo thabiti.
“Tume ya uchaguzi ni kipande cha mzaha,Inazalisha wapiga kura,” aliongeza, akionyesha mashaka juu ya dai la tume hiyo kwamba imesajili wapiga kura milioni 17 kutoka kwa idadi ya watu vijana wa milioni 33.
– Umaskini, ghasia –
Zaidi ya asilimia 74 ya watu wa Msumbiji walikuwa wanaishi katika umasikini mwaka 2023, kulingana na Benki ya Maendeleo ya Afrika.
Nchi hiyo ilikuwa na matumaini ya kupata ongezeko la uchumi kutokana na uvumbuzi wa akiba kubwa ya gesi kaskazini mwaka 2010, lakini ghasia za kigaidi katika mkoa wa Cabo Delgado, kaskazini kabisa, zilisababisha ExxonMobil na TotalEnergies kusitisha miradi yao. Uchumi utahitaji kuwa kipaumbele kwa serikali, alisema mchambuzi Aleix Montana.
“Rais mpya wa Msumbiji atalazimika kushughulikia viwango vya juu vya deni la umma na mapato duni, huku miradi muhimu ya nishati ikiendelea kukumbwa na kucheleweshwa kutokana na ghasia katika mkoa wa Cabo Delgado,” alisema.