Rais Museveni ampongeza Rais mteule wa Kenya, William Ruto

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amempongeza rais mteule wa Kenya, William Ruto, kwa ushindi wake katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati alimtangaza William Ruto kuwa mshindi jana Jumatatu, Agosti 15.

Rais Museveni alimsifu Bw Ruto kwa kushinda katika taarifa yake leo Jumanne, akimhakikishia kuimarishwa kwa uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.

“Kwa niaba ya Waganda wote, nampongeza Mheshimiwa Willaim Samoei Ruto kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa 5 wa Jamhuri ya Kenya,” alisema Museveni.

“Ningependa kuwahakikishia dhamira ya Uganda ya kuendelea kushirikiana na Kenya katika kuendeleza ajenda ya kikanda na bara kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki, Umoja wa Afrika na majukwaa mengine ya kimataifa.”

Pia alionyesha matumaini kuwa ushirikiano wake wa karibu na Ruto utatoa mafanikio makubwa kwa mataifa yote mawili.

“Ushirikiano wetu baina ya nchi mbili utapata mafanikio makubwa na ninatazamia kufanya kazi kwa karibu zaidi nanyi. Mungu ibariki Kenya. Mungu ibariki Afrika Mashariki.”

Viongozi wengine waliompengeza Ruto ni Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa na Rais wa zamani wa Somalia Mohamed Farmaajo.