Karua: ”Rais Ruto anatumia polisi kunyamazisha wakosoaji wake”

Kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua na Jaji Mkuu wa Kenya wa zamani Willy Mutunga sasa wanadai kikosi haramu cha polisi ndicho kinahusika na msururu wa visa vya utekaji nyara wa wakosoaji wa serikali.

Wawili hao pia wamemkosoa  Rais William Ruto kwa kutumia polisi kunyamazisha wakosoaji wake.

Wakiongea na wanahabari Jumapili baada ya kukamatwa kwa mwanaharakati Boniface Mwangi, Bi Karua alidai kuwa wamepata habari za kuaminika kuhusu uwepo wa kikosi fulani eneo la Karen, Nairobi, ambacho wanachama wake huwateka nyara watu na kutoweka nao.

Alidai kuwa kikosi hicho kinashirikisha maafisa wa jeshi na idara ya polisi walioagizwa kulenga vijana wanaoelezea kuchukizwa na utawala wa Ruto.

“Visa hivyo wa utekaji nyara na mauaji ya kiholela ya watoto wetu, haswa vijana wasio na hatia, sasa ndio kitambulisho cha utawala wa Ruto,” Bi Karua akasema.

Kufuatia kukamatwa kwa Bw Mwangi akiwa nyumbani kwake kaunti ya Machakos, Bi Karua na Dkt Mutunga wametaka aachiliwe huru.

Wito sasa na huo pia ulitolewa na Waziri wa zamani Dkt Mukhisa Kituyi, Mkurugenzi wa Shirika la Kislamu za Kutetea Haki za Kibinadamu (MUHURI) Khelef Khalifa na aliyekuwa Mbunge wa Mukurweini Kabando wa Kabando.

“Tunataka haki za wanaharakati nchini ziheshiwe,” akasema Bi Karua.

Alidai kuwa Bw Mwangi alikamatwa na polisi wenye silaha ambao hawakujitambulisha kwake na kwa watu wa familia yake.

“Kenya haifai kuwa nchi ambayo familia zinaishi kwa hofu kwamba wapendwa wao wanaweza kuchukuliwa usiku na wasirejee nyumbani. Haki ya uhai iliyoko katika Katioba inapasa kuzingatiwa kikamilifu wala sio kwa masharti fulani,” Bi Karua akasema.